Simba SC

SIMBA YATIKA KWA HASIRA MECHI YA KISASI DHIDI YA DODOMA JIJI

Vardo May 23, 2026 10:58 pm

KOCHA Msaidizi wa Simba SC, Selemani Matola, amesema mchezo wao dhidi ya Dodoma Jiji FC hautakuwa mwepesi hata kidogo, akibainisha kuwa maandalizi yao yote yamelenga kuhakikisha wanapata pointi tatu muhimu nyumbani.

Akizungumza kuelekea mtanange huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa Jumamosi, Matola amekumbusha ugumu walioupata kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa ugenini, ambapo Simba walilazimika kutoka sare ya bao 1-1.

Kocha huyo amesema matokeo hayo yamewafanya waingie kwenye mchezo wa marudiano kwa tahadhari zaidi.

“Haiwezi kuwa mechi rahisi. Mchezo wa kwanza walitupa ugumu mkubwa kwa sababu tulitoka sare ya 1-1 ugenini kwao,” amesema Matola.

Ameongeza kuwa kikosi kimejipanga vizuri na kinaendelea na maandalizi ya mwisho ili kuhakikisha kinatumia vizuri uwanja wa nyumbani kupata ushindi muhimu.

“Tunaelewa kabisa kwamba Dodoma Jiji si timu ya kubezwa. Tunajiandaa kuwavaa kwa nguvu zote ili tupate pointi tatu, ingawa tunajua haitakuwa rahisi,” ameongeza.

Matola pia ameeleza kuwa hali ya morali ndani ya kikosi iko juu, huku wachezaji wakiwa na kujiamini na umoja mkubwa unaowapa nguvu ya kupambana uwanjani.

“Morali ya wachezaji iko vizuri sana, uwezo na kujiamini vipo juu. Vipaji tulivyonavyo vinatupa jeuri nzuri kuelekea mchezo huu,” amesema.

Amesisitiza kuwa Simba inahitaji nidhamu na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi ili kuhakikisha pointi tatu zinabaki Dar es Salaam, huku macho yote yakielekezwa kwenye ushindi muhimu wa wikiendi hii.

OKELLO AZUA MJADALA YANGA, MABAO 9 LAKINI HAONI CHA AJABU JKT WAANGUSHWA, SIMBA QUEENS WAWEKA MKONO MMOJA KWENYE UBINGWA