Habari za michezo
MSIMU UNAFUNGWA KWA KISHINDO UTAMU UPO CHINI
Vardo
May 23, 2026
10:54 am
HAPA nchini, mvutano wa kukaa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara umeanza kushika kasi kwa Simba na Yanga, lakini pia bado kuna vita nyingine ya kumaliza nafasi nne za juu ikizihusisha Azam, Singida Black Stars, TRA United na JKT Tanzania.
Kule chini, KMC ni kama ndiyo imekubali kuwa ya kwanza kushuka ikikusanya pointi tisa ikibakiwa na mechi sita, lakini Tanzania Prisons, inapambana kujinasua hivi sasa ikishika nafasi ya 15 na pointi 17 kabla ya kucheza na Azam.
Juu yake kuna Mbeya City (pointi 22) na Coastal Union (pointi 25), hivi sasa zipo kwenye eneo la kucheza playoff ya kubaki kwenye ligi.
Wakati Ligi Kuu Bara hali ikiwa hivyo kwa maana ya ushindani upo juu, kati na chini, kule Ulaya utamu upo kati na chini, lakini kubwa zaidi ni chini kwa baadhi ya ligi ambapo wikiendi hii tunakwenda kushuhudia vicheko na vilio.
Rasmi wikiendi hii msimu wa soka wa 2025-2026 unahitimishwa kwa ligi tano maarufu Ulaya, pazia likitarajiwa kufungwa kwa vishindo huku kila ligi ikiwa tayari imeshatoa bingwa wake.
Huu umekuwa msimu wa kusisimua ambapo mabingwa wameshafahamika, lakini vita ya kuwania nafasi za kushiriki michuano ya Ulaya kwa maana ya Ligi ya Mabingwa, Europa League na Conference League zinakwenda kuamuliwa siku za mwisho. Pia mapambano ya kuepuka kushuka daraja bado ni mbichi katika baadhi ya ligi.
PREMIER LEAGUE
Ligi Kuu ya England msimu huu imeshuhudiwa Arsenal ikitwaa ubingwa baada ya mchuano mkali tangu mwanzo.
Hadi kufikia raundi ya 37, Arsenal imekusanya pointi 82, ikifuatiwa na Manchester City yenye pointi 78. Hii ina maana Arsenal imechukua ubingwa kwa tofauti ya pointi 4 dhidi ya mpinzani wake wa karibu.
Ikiwa wikiendi hii tunashuhudia kuhitimishwa kwa msimu, tayari Arsenal, Manchester City, Manchester United (pointi 68), na Aston Villa (pointi 62) ambazo zote zipo nafasi nne za juu kwenye msimamo, zimejihakikishia kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
England msimu ujao kutakuwa na timu nane zitakazoshiriki michuano ya Ulaya ambapo tano za juu zitakuwa Ligi ya Mabingwa, mbili zinazofuatia kwa maana ya nafasi ya sita na saba zitashiriki Europa League na ya nane Conference League.
Hivi sasa vita imebaki kwenye nafasi moja ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya kukamilisha idadi ambapo Liverpool (pointi 59) inahitaji pointi moja tu kujihakikishia kumaliza ya tano kwani ikishindwa kupata ushindi, Bournemouth (pointi 56) inaweza kuipiku ikishinda. Tofauti ya pointi tatu inazitenganisha timu hizo, lakini bado Liverpool ina wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa, hivyo ikitokea mechi ya mwisho imepoteza kwa idadi kubwa ya mabao kisha mshindani wake naye akapata ushindi mnono, tutashuhudia maajabu.
Pia kwenye eneo la Europa League, Brighton (pointi 53) inahitaji kushinda kuikimbia Chelsea (pointi 52) ambazo zinachuana vikali. Kwa sasa Chelsea ina uhakika wa kushiriki Conference League, huku pia ikiwa na uwezo wa kucheza Europa League kama Brighton akizingua.
Kwa upande mwingine, Erling Haaland (Man City) anaongoza kwa ufungaji akiwa na mabao 27 katika mechi 35, akifuatiwa na Igor Thiago wa Brentford mwenye mabao 22. Antoine Semenyo (16) na João Pedro (15) wanakamilisha orodha ya juu. Haaland anaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kuwa mfungaji bora.
Kinara wa asisti ni Bruno Fernandes wa Manchester United akiwa nazo 20 katika mechi 34, akitengeneza nafasi za wazi mara 132. Anafuatiwa na Rayan Cherki (12) na Jarrod Bowen (10). Bruno amefikia rekodi ya asisti nyingi katika msimu mmoja wa Premier kama alivyofanya Thierry Henry (2002-2003) na Kevin De Bruyne (2019-2020).
Kipa wa Arsenal, David Raya ana cleansheets 19, ndiye kinara huku rekodi hiyo amelingana na aliyekuwa kipa wa timu hiyo, David Seaman msimu wa 1993-1994 na 1998-1999.
Timu za Burnley (pointi 21) na Wolves (pointi 19) tayari zimeshashuka daraja. Nafasi moja ya mwisho inazihusu West Ham United (pointi 36) na Tottenham Hotspur (pointi 38).
Jumapili hii katika mechi za kuhitimisha ligi hiyo ambapo zote zitaanza saa 12:00 jioni, mmoja kati yao atashuka hivyo mechi ambayo Tottenham itaikaribisha Everton na ile ya West Ham dhidi ya Leeds United, itatolewa macho zaidi kuona nani atabaki, kisha nani ataungana na Burnley na Wolves.
SERIE A
Nchini Italia, Inter Milan imethibitisha ubora wake kwa kutwaa taji lao la 21 la Serie A mapema mnamo Mei 3, 2026.
Hadi raundi ya 37, Inter imekusanya pointi 86, huku Napoli ikiwa na pointi 73 katika nafasi ya pili. Hii ni tofauti kubwa ya pointi 13 kati ya bingwa na nafasi ya pili. Timu hizo ndizo zina uhakika wa kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.
Kutoka Serie A, zimebaki nafasi mbili kukamilisha timu nne za kucheza michuano hiyo ya Ulaya ambapo sasa AC Milan (pointi 70), Roma (pointi 70), Como (pointi 68) na Juventus (pointi 68), zinatolea macho mechi za mwisho kujihakikisha nafasi hiyo.
Atalanta yenye pointi 58, tayari imefuzu Conference League, hivyo timu hizo nne za AC Milan, Roma, Como na Juventus zinaingia wikiendi hii kwa hesabu kali. Atakayeteleza, ataikosa UEFA na kushiriki Europa League.
Lautaro Martínez wa Inter Milan, ndiye kinara wa mabao akiwa nayo 17. Marcus Thuram, Tasos Douvikas na Donyell Malen wanafuata wakiwa na 13 kila mmoja. Martínez suala la kuwa mfungaji bora lipo karibu sana.
Jean Butez wa Como anaongoza kwa clean sheets akiwa nazo 19, hii inamaanisha kwamba yeye ndiye kinara wa msimu huu kwani hakuna wa kumzidi kutokana na kwamba anayefuatia Mile Svilar (17) na Yann Sommer (15) huku mechi ikibaki moja.
Timu za Hellas Verona (pointi 21) na Pisa (pointi 18) tayari zimeshashuka daraja. Vita ya kubaki ipo kwa Lecce (pointi 35) na Cremonese (pointi 34).
Como vs Cremonese, Lecce vs Genoa na Torino vs Juventus, ni mechi ambazo zinatolewa macho zaidi kutokana na kila timu kuhitaji ushindi wa kukaa sehemu nzuri.
Mechi za kuhitimisha msimu wa Serie A, Ijumaa imepigwa moja, Jumamosi zitachezwa zingine, kisha Jumapili ndiyo mwisho.
LA LIGA
Nchini Hispania, Barcelona imerejea kutawala kwa kutwaa taji la 29 ndani ya La Liga mapema kwenye raundi ya 35.
Hadi raundi ya 37, Barcelona ina pointi 94, huku Real Madrid ikiwa na pointi 83, tofauti ya pointi ni 11.
Hispania imepata nafasi tano za Ligi ya Mabingwa Ulaya zilizochukuliwa na Barcelona, Real Madrid, Villarreal (pointi 69), Atletico Madrid (pointi 69) na Real Betis (pointi 57). Real Sociedad (mabingwa wa Copa del Rey) watawakilisha katika Europa League, huku Getafe (pointi 48) wakishikilia nafasi ya Conference League, lakini kama wakishinda mechi ya mwisho kisha Celta Vigo (pointi 51) ikapoteza, basi zitapishana. Celta Vigo inatakiwa kushinda au kupata sare kujihakikishia kucheza Europa League.
Kylian Mbappé anaongoza akiwa na mabao 24 katika mechi 30, akifuatiwa kwa ukaribu na Vedat Muriqi (Mallorca) mwenye mabao 22. Tofauti ya mabao mawili inafanya mechi ya mwisho kila mmoja kupambana kuwa mfungaji bora.
Lamine Yamal wa Barcelona anaongoza akiwa na pasi za mabao 11, akifuatiwa na Luis Milla (10).
Joan García wa Barcelona ndiye kipa bora akibeba tuzo ya Zamora kufuatia kuruhusu mabao 21 katika michezo 30 (wastani wa 0.7).
Real Oviedo (pointi 29) tayari imeshuka daraja. Vita ya kuepuka nafasi mbili zilizobaki ni kali kati ya Mallorca (pointi 39), Girona (pointi 40), Elche (pointi 42), Osasuna (pointi 42) na Levante (pointi 42).
Kuna uhondo mkubwa katika eneo la kushuka daraja kwani baadhi ya mechi inakutanisha wote wanaohitaji ushindi ili kuwa salama. Ratiba ya mechi za kuvutia ni Mallorca vs Real Oviedo, Girona vs Elche na Getafe vs Osasuna.
Uhondo wote huu utashuhudiwa Jumamosi hii kwa kuchezwa mechi tisa, kisha Jumapili itamaliziwa moja.
LIGUE 1
Ligi ya Ufaransa tayari imekamilisha msimu wake mnamo Mei 17, 2026. PSG imekuwa bingwa kwa mara ya 14 ikikusanya pointi 76, huku RC Lens ikimaliza ya pili na pointi 70, tofauti ikiwa ni 6.
Zilizofuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya ni PSG, Lens, Lille (pointi 61) na Olympique Lyon (pointi 60). Marseille (pointi 59) itashiriki Europa League na Stade Rennais (pointi 59) imekata tiketi ya kucheza Conference League.
Hata hivyo, Stade Rennais inaweza kushiriki Europa League kama itatwaa Coupe de France 2025–26 ambapo fainali itacheza dhidi ya Lens yenye uhakika wa kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Mfungaji Bora ameibuka Estéban Lepaul wa Rennes aliyefunga mabao 21. Joaquín Panichelli na Mason Greenwood wamefuata na mabao 16 kila mmoja.
Adrien Thomasson wa Lens, kinara wa pasi za mabao akiwa nazo 10, wakati Robin Risser pia wa Lens, amechaguliwa kuwa kipa bora, huku PSG ikiwa na safu bora ya ulinzi iliyoruhusu mabao 29 pekee.
FC Nantes na FC Metz zimeshashuka daraja moja kwa moja. Nice italazimika kucheza mechi za mchujo dhidi ya AS Saint-Etienne kusalia ligi kuu. Huku kazi imeshaisha.
BUNDESLIGA
Bayern Munich wamerejesha heshima nchini Ujerumani kwa kutwaa ubingwa kwa mara ya pili mfululizo baada ya ule wa 2023–2024 Bayer Leverkusen kuwa bingwa.
Timu hiyo ilijihakikishia ubingwa kwenye raundi ya 30 baada ya kuifunga Stuttgart 4-2. Timu nyingine zilizofuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya ni VfB Stuttgart, Borussia Dortmund na Bayer Leverkusen.
Mfungaji Bora ni Harry Kane akifunga mabao 36 katika mechi 31. Nyuma yake ni Deniz Undav (19) na Serhou Guirassy (17).
Kinara wa pasi za mabao ni Michael Olise wa Bayern akiwa na 19, akifuatiwa na Julian Ryerson (15).
Timu za FC Heidenheim na FC St. Pauli zimeshashuka daraja moja kwa moja, wakati VfL Wolfsburg, Mei 25 mwaka huu inarudiana na SC Paderborn katika play off ya kucheza Bundesliga msimu ujao baada ya mechi ya kwanza kutoka 0-0. Msimu wa ligi hii umefikia tamati tayari.
SAUDI PRO LEAGUE
Ukiweka kando ligi tano maarufu Ulaya, pia msimu huu imeshuhudiwa mashabiki wa soka wakifuatilia Ligi Kuu ya Saudi Arabia kwa mara nyingine kutokana na uwepo wa mastaa mbalimbali waliowahi kucheza Ulaya akiwemo Cristiano Ronaldo na Karima Benzema.
Msimu wa ligi hiyo ulihitimishwa Mei 21, 2026, kwa namna ya kusisimua Alhamisi Mei 21, 2026.
Al-Nassr anayocheza Ronaldo na Sadio Mane, imetawazwa mabingwa ikiwa na pointi 86, ikiwapiku mabingwa watetezi Al-Hilal waliomaliza na pointi 84 (tofauti ya pointi 2). Huu ni ubingwa wa kwanza wa ligi kwa Cristiano Ronaldo nchini humo.
Huu ulikuwa ubingwa wa 11 wa ligi kwa Al-Nassr katika historia yao na taji lao la nne tangu kuanzishwa kwa mfumo wa sasa wa Saudi Pro League. Ushindi huu ulikuwa na maana kubwa kwa sababu imekuwa mara ya kwanza kwa Al-Nassr kuchukua ubingwa tangu msimu wa 2018-19, ikimaliza kipindi cha miaka saba ya kukosa taji ikiwemo kumaliza nafasi ya pili katika misimu miwili iliyopita.
Mfungaji Bora amekuwa Julián Quiñones wa Al-Qadsiah akifunga mabao 33, akifuatiwa na Ivan Toney (32) na Cristiano Ronaldo (28). Kinara wa pasi za mabao ni Joao Felix wa Al-Nassr akiwa nazo 13.
Timu zilizoshuka daraja ni Damac FC (pointi 29), Al-Okhdood (pointi 20) na Al-Najma (pointi 16).