Simba SC
Simba SC

KUHUSU BAJABER ‘KUPIGWA PANGA’ SIMBA….BARKER KAMTAZAMA WEE..KISHA AKASEMA HILI….

admin May 23, 2026 1:54 pm

WAKATI maswali yakiendelea kuwa mengi kuhusu hatma ya kiungo Mohamed Bajaber, Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker amesema kwenye hesabu zake za msimu ujao nyota huyo yupo, lakini kuna mambo ameyazungumza yatakayoamua jambo hilo.

Baada ya kupotea uwanjani kwa sababu ya majeraha huku jina lake likichomolewa katika usajili wa nyota wanaotumika kwa mashindano yaliyopo chini ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), tangu kufungwa kwa dirisha dogo la Januari 2026, Bajaber alirudi dimbani Aprili 22, 2026 aliposafiri na kikosi cha Simba kwenda Zanzibar kushiriki Kombe la Muungano 2026 na kuisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa huku akicheza michezo kadhaa ukiwemo ule wa fainali dhidi ya Yanga.

Bajaber amerejea uwanjani hivi karibuni baada ya kukabiliwa na mfululizo wa majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu tangu aliposajiliwa mwanzoni mwa msimu huu.

Nyota huyo raia wa Kenya, aliondolewa kwenye mfumo wa usajili wa mashindano kutokana na majeraha ya paja, lakini kocha alimrudisha kikosini kwa ajili ya michuano ya Kombe la Muungano yaliyofanyika kule Zanzibar mwezi Aprili 2026 ili kuangalia maendeleo yake.

Ikumbukwe kuwa, baada ya kusajiliwa Agosti 2025, Bajaber aliumia misuli ya paja akiwa na timu ya taifa ya Kenya maarufu Harambee Stars. Baadaye, Januari 18, 2026, aliumia tena paja la kushoto baada ya kucheza dakika 12 tu dhidi ya Mtibwa Sugar katika Ligi Kuu Bara.

Kabla ya kuumia mfululizo, alifunga bao lake la kwanza la Ligi Kuu Bara katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Mbeya City, Desemba 04, 2025.

Mwanaspoti iliwahi kuandika kuwa, mustakabali wake ndani ya Simba kwa msimu ujao bado uko shakani, huku kukiwa na klabu kutoka Kenya zinazofuatilia hali yake akiwa tayari anaelekea kumaliza mwaka mmoja ndani ya Simba aliposaini miaka miwili akitokea Kenya Police.

Akizungumzia kuhusu hilo, Barker amesema anatamani kumuona Bajaber tena ndani ya kikosi cha Simba msimu ujao, ingawa anataka apate uhakika wa jambo moja kubwa ambalo hataki lijirudie likawa kama kosa tena.

“Bajaber ni mchezaji mzuri sana na hilo linafahamika, nataka kumuona akiendelea kuitumikia Simba msimu ujao ila shida ni kuhusu kupona kwa majeraha ambayo yalimzuia msimu huu.

“Jambo la kulizingatia na ninalifuatilia sana ni kuhusu uimara wa Bajaber hasa upande wa majeraha kama hilo litathibitika yuko sawa kabisa, basi msimu ujao hakutakuwa na kipingamizi cha yeye kurudi Simba,” amesema Barker.

MSIMU UNAFUNGWA KWA KISHINDO UTAMU UPO CHINI UKWELI USIOSEMWA HUU HAPA….NYUMA YA SIMBA HII YA MOTO KUNA HUYU JAMAA….