UKWELI USIOSEMWA HUU HAPA….NYUMA YA SIMBA HII YA MOTO KUNA HUYU JAMAA….
KWA miaka minne sasa ulikuwa ukiuliza juu ya timu gani itachukua ubingwa jibu linakuwa rahisi itatajwa Yanga, halikuwa jibu ambalo lingesumbua kutokana na ubora wa kikosi chao ukilinganisha na wale ambao anashindana nao.
Msimu huu mambo yamebadilika, hasa kuanzia mzunguko wa pili ambapo Simba ambayo ilikuwa haipewi nafasi imeibuka ikitaka kurudisha heshima yake kwenye kuchukua mataji ikionyesha mabadiliko makubwa.
Simba ilianza mageuzi hayo juu yake akiwa Crescentius Magori ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ambaye baada ya kuanza kwa kuyumba kidogo miezi ya kwanza sasa mambo yamebadilika, Wekundu hao chini yake wanaonyesha kwamba sasa timu inakwenda kujipata.
PANTEV KATOKA, BARKER KAINGIA
Magori alipotua Simba tu kama mwenyekiti wa bodi, alikutana na presha ya kuondoka kwa aliyekuwa kocha wa timu hiyo Fadlu Davids, ambaye msimu uliopita alitangulia kufanya kazi nzuri ya kutengeneza kikosi imara.
Msimu huu ulipoanza Fadlu akashtua kwa kuomba kuondoka akirejea nchini Morocco kujiunga na timu yake ya zamani ya Raja Athletic, uamuzi huo ukailazimisha Simba kuingia sokoni kisha ikamchukua kwa haraka kocha Dimitar Pantev.
Hata hivyo, ujio wa Pantev ulionyesha ni kama Simba haikufanya maamuzi sahihi kwani baada ya miezi miwili iliachana na kocha huyo, kisha akashushwa Steve Barker ambaye alikuwa kocha mwenye uzoefu mkubwa ambaye kwa sasa anaendelea kuiimarisha timu hiyo ikiwa tishio.
Barker hapa ndani hajapoteza mchezo wowote kwenye mashindano ya ndani ambapo matokeo yake mabaya yamekuwa ni kupata sare tano pekee kati ya saba za wekundu hao, akionyesha kwamba ameipatia timu hiyo.
KUJILIPUA JANUARI
Simba chini ya Magori ikafanya maamuzi magumu wakati wa dirisha dogo la usajili Januari ni kama ilivua injini kisha kuvalisha nyingine mpya ikiacha mastaa na kusajili wengine wapya hatua ambayo wakati mwingine ni ngumu sio kila timu inaweza kufanya hivyo
Simba Januari iliwaacha mastaa wake nane wakiwemo, Steve Mukwala, Jean Charles Ahoua, Mohammed Bajaber, Kibu Denis ambao waliuzwa Libya, Chamou Karaboue, Joshua Mutale, Mzamiru Yassin, Awesu Awesu.
Hapo hapo ikaingiza wengine wapya nane ambao ni kipa Djibril Kasali, Nickson Kibabage, Baraka Mwangosi,Ismael Toure, Lebase Gueye, Anicet Oura, Inno Loemba na Clatous Chama kuja kukiongezea nguvu kikosi hicho.
Ujio wa wachezaji hao ukiongeza na wale ambao waliwakuta iliifanya Simba kuwa na kikosi imara kuanzia mzunguko wa pili ikionyesha mpira mzuri uwanjani na kuanza kufufua hesabu za kutimia malengo yake.
Hesabu hizo zikaanza kulipa baada ya wekundu hao kuchukua taji la kwanza msimu huu ikiifunga Yanga kwa bao 1-0 kwenye Fainali ya Kombe la Muungano, ikishusha presha kwamba safari ya mageuzi ni kama inawezekana.
KURUDISHA KAMATI YA MASHINDANO
Utawala wa Magori akiwa mwenyekiti wa bodi hiyo ukafanya mabadiliko mengine ukifufua nguvu ya kamati ya mashindano ya Wekundu hao ikiwa na vigogo mbalimbali lakini moja ya sura mpya ilikuwa ni uwepo wa Swedy Mkwabi ambaye alirudishwa ndani ya bodi ya wakurugenzi wa klabu hiyo akiteuliwa na rais wa heshima wa Simba Mohammed Dewji ‘MO’.
Ukiacha nafasi hiyo Magori alipokalia kiti hicho akaunda kamati ya mashindano ambayo mwenyekiti wake ni Mkwabi ambapo ilikwenda kuchangamsha usimamizi wa kikosi hicho kwenye mechi mbalimbali na matokeo yakipatikana.
CHAMA NA MOTO WAKE
Wakati Clatous Chama anaondoka Simba mwaka mmoja uliopita akiwa mchezaji huru, viongozi wengi wa Wekundu hao waliona kama Mzambia huyo zama zake zimekwisha na umri umemtupa mkono, akaenda kujiunga na Yanga ambapo hakufanya makubwa.
Baada ya Yanga kumalizana na Chama kufuatia mkataba wao wa mwaka mmoja kumalizika, Mzambia huyo alitua Singida alikocheza mzunguko wa kwanza, Magori wakati anaitafuta Simba mpya akamrudisha Mzambia huyo.
Kumbuka Chama wakati anatua Simba kwa mara ya kwanza alikuja kipindi ambacho Magori alikuwa ndiye Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, hakuna ambaye alitarajia kama Chama angeweza kuongeza kitu kikubwa ambacho anakifanya sasa akifunga mabao manane na asisti sita na kumfanya kiungo huyo kuhusika kwenye jumla ya mabao 14.
SIMBA NJIA YA MATAJI
Simba sasa inayataka makombe mawili yaliyosalia, ikifanikiwa kupunguza tofauti ya pointi kati yake na Yanga kutoka tano mpaka sasa kusalia mbili kama Yanga jana ilishinda kwenye mchezo wake dhidi ya Singida lakini kama haitoshi imetinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB ikitarajiwa kupambana na Coastal.
HESHIMA YA DABI
Kama kuna timu ambayo inaipa Yanga presha kubwa kwa sasa ni Simba ambayo inatishia ubabe wa mabingwa hao watetezi kwenye mataji lakini kubwa zaidi ni kwamba wekundu hao wameshafuta woga wa kucheza na watani wake baada ya mechi tatu za mwisho ikitoa sare mbili na kushinda moja.
Simba ni kama imelipa kisasi baada ya kupoteza mchezo wa fainali ya Ngao ya jamii ikiifunga Yanga kwenye fainali ya Muungano na mechi mbili za ligi zikimalizika kwa sare wekundu hao wakiendelea kuonyesha hatua sahihi za kujipata.