Simba SC

VITA YAONGEZEKA LIGI KUU, OKELLO AIPA PRESHA SIMBA

Vardo May 28, 2026 4:31 pm

MBIO za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara zikizidi kupamba moto, kiungo mshambuliaji wa Yanga SC, Allan Okello, ameweka wazi msimamo wa kikosi hicho kuelekea hatua za lala salama za msimu, akisisitiza kuwa dhamira yao ni moja tu kutwaa ubingwa.

Okello amesema anaelewa ugumu mkubwa uliopo katika ligi ya msimu huu, hasa kutokana na timu zote kuongeza kasi na ubora kadri msimu unavyokaribia ukingoni. Hata hivyo, amesisitiza kuwa Yanga iko tayari kwa kila changamoto inayojitokeza.

“Ligi ni ngumu ila tunajua cha kufanya. Tunaamini tutashinda michezo yote na tutakuwa mabingwa. Si rahisi kwa sababu timu zinaimarika tunapoelekea mwisho wa msimu, lakini imani yetu ni kwamba tutaendelea kupambana kwenye kila mchezo tupate alama tatu, ipo ndani ya uwezo wetu,” amesema Okello.

Nyota huyo ameongeza kuwa mafanikio ya timu yanategemea kiwango cha juu cha kujituma katika kila mchezo, sambamba na kuheshimu wapinzani wote wanaokutana nao uwanjani.

“Pale tunapotoa kila kitu na kujitoa kwa asilimia mia na kuwaheshimu kila mpinzani tunaamini tutashinda kila mchezo,” ameongeza.

Okello hakusita kugusia ushindani mkali unaotokana na wapinzani wao wa jadi, Simba SC, akisema nao ni miongoni mwa timu zenye uwezo mkubwa wa kufanya vizuri katika michezo yao iliyosalia.

Amesema hali hiyo inazidi kuifanya ligi kuwa ngumu zaidi, lakini Yanga inaendelea kuzingatia kila mchezo mmoja baada ya mwingine huku lengo likiwa ni kukusanya pointi tatu muhimu katika kila hatua kuelekea kutimiza ndoto yao ya ubingwa msimu huu.

HATMA YA IBENGE YAZUA MTIKISIKO AZAM FC MOTO WAIBUKA SIMBA SC, MALENGO MAWILI PRESHA NZITO MWISHO WA MSIMU