Michezo Bongo

BARNABAS AFICHUA JAMBO TRANSIT CAMP

Vardo June 1, 2026 7:49 pm

KOCHA wa Transit Camp, Vicent Barnabas amesema makosa binafsi wanayoyafanya katika mechi mbalimbali ndiyo yanayochangia mwenendo usioridhisha kwa kikosi hicho cha maafande msimu huu, japo wataendelea kuonyesha ushindani kwa wapinzani wao.

Akizungumza na Soka la bongo, Barnabas amesema kuna ongezeko la makosa ya mchezaji mmoja mmoja katika timu hiyo, ingawa ni suala analoendelea kulifanyia kazi kwa haraka, ili watimize malengo ya kumaliza wakiwa nafasi nne za juu kwenye msimamo.

“Bado tuna uwezo wa kumaliza nafasi nne za juu na kupata fursa ya kucheza mechi za ‘Play-Off’ kuwania kupanda Ligi Kuu, ni jambo linalowezekana ila tunahitaji kuongeza umakini kuanzia eneo la kujilinda na la ushambuliaji,” amesema Barnabas.

Awali, Barnabas alikuwa ni kocha msaidizi ingawa amepewa majukumu hayo baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Shadrack Nsajigwa ‘Fuso’, kuondoka na kwenda kujiunga na maafande wa Tanzania Prisons, akichukua nafasi ya Mkenya Zedekiah ‘Zico’ Otieno.

Barnabas ni miongoni mwa makocha wenye rekodi za kuvutia katika soka la Tanzania na aliipa timu ya vijana ya Mtibwa Sugar chini ya miaka 20, mataji matano mfululizo, kuanzia mwaka 2018 hadi 2022, baada ya kuichezea pia kwa mafanikio.

Kabla ya kujiunga na kikosi hicho cha maafande wa Transit Camp, msimu uliopita wa 2024-2025, Barnabas aliipa pia ubingwa timu ya Yanga chini ya miaka 17, baada ya kuachana na Mtibwa Sugar, akiendeleza rekodi bora kwa kila timu anayofundisha.

Kikosi hicho kabla ya mechi ya jana dhidi ya B19 FC, kimecheza 26, ambapo kimeshinda 15, kikitoka sare nne na kupoteza saba, kikishika nafasi yake ya tano na pointi zake 49, huku safu hiyo ya ushambuliaji ikifunga mabao 38 na kuruhusu 28.

TURKEY KUJIPIMA NGUVU NA NORTH MACEDONIA, MAANDALIZI YA WC 2026 NAMUNGO YAANZA HESABU ZA VIDOLE LIGI KUU