NAMUNGO YAANZA HESABU ZA VIDOLE LIGI KUU
WAKATI presha ya kukwepa kushuka daraja ikizidi kuongezeka, Namungo imeanza kufanya hesabu za kujinusuru baada ya kuweka lengo la kukusanya angalau pointi tisa katika mechi tano zilizobaki.
Namungo, iliyopanda Ligi Kuu msimu wa 2019/20 kabla ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika, kwa sasa ipo katika mazingira magumu baada ya kucheza mechi 13 mfululizo bila ushindi.
Timu hiyo ya Lindi ipo nafasi ya 13 ikiwa na pointi 25.
Akizungumza na Soka la Bongo, kiungo Helbert Lukindo alisema pamoja na ugumu wa msimu huu, bado wanaamini wana uwezo wa kubaki Ligi Kuu.
“Kwa hali ya ushindani ilivyo, tunahitaji kushinda mechi zote zilizobaki. Lakini hata tukishindwa kufanya hivyo, pointi tisa zinaweza kutufikisha pointi 34 ambazo zinaweza kutuweka salama,” alisema Lukindo.
Aliongeza kuwa mechi tatu za nyumbani zilizobaki zinawapa matumaini makubwa ya kufanikisha malengo yao na ikiwezekana kuzoa pointi zote tisa.
Namungo ambayo inafundishwa na kocha Juma Mgunda ilianza msimu kwa kasi ikikaa kileleni kwa vipindi vifupi lakini sasa ipo kwenye wakati mgumu kwenye msimamo.