KOMBE LA DUNIA LAICHEZESHA SIMBA MCHANA
WAKATI Ligi Kuu Bara ikiendelea kupamba moto, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imefanya mabadiliko ya ratiba ya mchezo wa Mbeya City dhidi ya Simba ambao awali ulipangwa kuchezwa Juni 18, hata hivyo Kombe la Dunia limechangia.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya TPLB, mchezo huo namba 214 wa Ligi Kuu sasa utachezwa Juni 17, 2026 katika Uwanja wa Sokoine kuanzia saa 8:00 mchana badala ya saa 10:00 jioni kama ilivyopangwa awali.
TPLB imeeleza kuwa uamuzi huo umefikiwa kutokana na sababu za kiuendeshaji, bila kuweka wazi kwa undani sababu zilizochangia kubadilishwa kwa muda wa mchezo huo.
“Bodi ya Ligi inakutaarifu kuwa imefanya mabadiliko ya muda wa mchezo tajwa hapo juu. Mchezo huo sasa utafanyika saa 8:00 mchana badala ya saa 10:00 jioni kama ilivyokuwa imepangwa awali,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Simba kucheza mechi ya Ligi Kuu katika muda huo, huku vigogo hao pamoja na Yanga wakiwa hawajawahi kucheza mechi ya ligi saa 8:00 mchana. Hata hivyo, chanzo cha ndania kinasema kuwa mechi hiyo imepelekwa saa nane mchana ili kutoingiliana na michezo ya Kombe la Dunia 2026 ambayo inaanza Juni 11 hadi Julai 19. “Fifa hawataki mashindano yao yaingiliane na michuano mingine yoyote, kiuhalisia ligi ilitakiwa kuwa imeshamaliza baada ya Juni 11, hivyo hawataki mechi yoyote iingiliane na michuano hiyo na TFF walikuwa wanafahamu hilo.
Wanataka kila shabiki mawazo yake yawe kwenye Kombe la Dunia tu ndiyo sababu ya mchezo huu kupigwa saa 8:00,’’ kilisema chanzo hicho. Mbeya City itakuwa na kazi ya kutumia vyema uwanja wake wa nyumbani mbele ya Simba inayopambana kuhakikisha inafanikisha malengo yake ya kutwaa ubingwa wa ligi. Mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kutokana na umuhimu wake kwa pande zote mbili.