Habari za michezo

PSG YATETEA TAJI LA ULAYA KUICHAPA ARSENAL KWA PENALTI

Vardo June 1, 2026 2:46 pm

PARIS Saint-Germain (PSG) imefanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kuichapa Arsenal kwa mikwaju ya penalti katika fainali iliyopigwa jijini Budapest nchini Hungary leo Mei 30, 2026.

Mchezo huo ulimalizika kwa sare ya bao 1-1 baada ya dakika 120 za ushindani mkali, kabla ya mabingwa hao wa Ufaransa kuibuka na ushindi kwenye changamoto ya mikwaju ya penalti.

Arsenal ilianza vyema mechi hiyo baada ya mshambuliaji Kai Havertz kuifungia bao la kuongoza dakika ya sita, na kuwapa mashabiki wa klabu hiyo matumaini ya kutwaa taji lao la kwanza la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Hata hivyo, PSG walirejea mchezoni kipindi cha pili baada ya Khvicha Kvaratskhelia kuangushwa ndani ya eneo la hatari na Cristhian Mosquera, mwamuzi akatoa penalti. Ousmane Dembele hakufanya makosa kutoka eneo la penalti na kusawazisha mchezo.

Timu hizo zilishindwa kupata bao la ushindi katika muda wa kawaida na ule wa nyongeza, hivyo mshindi kulazimika kupatikana kupitia mikwaju ya penalti.

Katika hatua hiyo ya uamuzi, Eberechi Eze wa Arsenal alikosa penalti yake ya kwanza kwa kupiga nje ya lango, huku kipa David Raya akiirejesha matumaini ya Arsenal baada ya kuokoa mkwaju wa Nuno Mendes wa PSG.

Hata hivyo, baada ya Lucas Beraldo kufunga penalti muhimu kwa PSG, beki Gabriel Magalhaes alikosa mkwaju wake kwa kuupiga juu ya lango, jambo lililowapa PSG ushindi na kutetea taji lao la Ulaya kwa penalti 4-3.

Matokeo hayo yanaifanya Arsenal kuendelea kusubiri taji lao la kwanza la Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku ndoto yao ya kuunganisha ubingwa wa Ligi Kuu England walioutwaa msimu huu na ubingwa wa Ulaya ikizimika kwa maumivu makubwa.

“Ni pigo kubwa kwetu baada ya msimu mzuri tuliokuwa nao, lakini tunapaswa kujifunza na kurejea tukiwa imara zaidi,” amesema nahodha wa Arsenal, Martin Odegaard baada ya mchezo huo.

Kwa upande wa PSG, ushindi huo unathibitisha ubora wao barani Ulaya na kuifanya klabu hiyo kuendelea kutawala soka la bara hilo baada ya kutetea kwa mafanikio taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

WAWI STARS, CHIPUKIZI FAINALI FA PEMBA