WAWI STARS, CHIPUKIZI FAINALI FA PEMBA
BINGWA mtetezi wa Kombe la FA Kanda ya Pemba, Chipukizi United, itakutana na Wawi Stars katika fainali ya michuano hiyo mwaka huu.
Chipukizi ilitinga hatua hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mwenge katika mchezo wa nusu fainali uliopigwa Uwanja wa Gombani, Pemba, jana.
Katika pambano hilo lililokuwa na ushindani mkubwa kwa dakika zote 90, Chipukizi ilitumia vyema nafasi zake za kushambulia na kufanikiwa kupata bao la ushindi.
Bao pekee la mchezo huo lililofungwa na mshambuliaji Faki Mwalimu, lililotosha kuipeleka timu hiyo fainali na kuizima ndoto ya Mwenge iliyokuwa ikisaka tiketi ya hatua hiyo.
Kwa upande wa Wawi Stars, ilifuzu fainali baada ya kuichapa Chake Chake mabao 4-0 katika mchezo mwingine wa nusu fainali.
Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Khamis Hamad Juma, amesema tarehe ya mchezo wa fainali itatangazwa baada ya kukamilika kwa hatua ya nusu fainali.
Amesema imekuwa vigumu kutangaza tarehe hiyo mapema kutokana na ratiba ya Chipukizi United kuwa na mechi za ligi zinazokaribiana.
“Tulipanga kutangaza tarehe ya fainali mapema, lakini changamoto iliyopo ni ratiba ya mechi za Chipukizi kuwa karibu sana. Hivyo, bado tupo kwenye mchakato wa kupanga tarehe inayofaa,” amesema.
Bingwa wa Kanda ya Pemba atacheza na bingwa wa Kanda ya Unguja kuwania ubingwa wa Zanzibar na tiketi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa. KMKM ndiyo bingwa mtetezi wa Zanzibar.