KOCHA UHAMIAJI APATA DAWA ZPL
WAKATI Uhamiaji ikipitia kipindi kigumu cha matokeo baada ya kucheza mechi sita mfululizo bila ushindi, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdul Saleh, amesema amepata suluhu ya changamoto zilizokuwa zikiikabili timu yake.
Akizungumza na Soka la Bongo, Abdul amesema amebaini kuwa eneo la ushambuliaji na umaliziaji lilikuwa tatizo kubwa kwa timu hiyo na tayari amelifanyia kazi.
Amesema eneo hilo ndilo lililokuwa likimsumbua zaidi, lakini anaamini maboresho yaliyofanyika yataanza kuonekana katika mechi zijazo.
“Tatizo kubwa lilikuwa kwenye umaliziaji, lakini tumelifanyia kazi kwa kiwango kikubwa. Tunaamini mabadiliko yataonekana katika mechi zijazo,” amesema.
Kocha huyo alisisitiza kuwa Uhamiaji bado haijatoka kwenye mbio za kumaliza katika nafasi nne za juu za msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar kutokana na uwezo walionao.
Abdul amesema mafanikio waliyoanza kuyaonyesha mwanzoni mwa msimu hayakuja kwa bahati mbaya, bali yalitokana na kazi kubwa ya kuwajenga wachezaji kisaikolojia baada ya kupitia kipindi kigumu msimu uliopita.
“Baada ya kumaliza vibaya msimu uliopita, wachezaji wengi hawakuwa sawa kisaikolojia. Tulitumia mbinu mbalimbali za kuwajenga upya ili warejee kwenye kiwango chao na kucheza soka la ushindani,” amesema.
Ameongeza kuwa hataki hali hiyo kujirudia, ndiyo maana aliamua kusajili wachezaji vijana wenye vipaji na ari kubwa ya kufanya vizuri.
Kocha huyo amefichua kuwa vijana hao wamekuwa chachu ya mabadiliko ndani ya timu, jambo ambalo limeanza kuzaa matunda na kurejesha imani kwa viongozi pamoja na mashabiki ambao wameendelea kutoa sapoti kubwa kwa timu hiyo.
Hiyo kwa sasa inapambana kumaliza nafasi nne za juu ili kupata nafasi ya kushiriki Kombe la Mapinduzi mwakani.