Michezo Bongo

JKU BADO INA MATUMAINI YA UBINGWA EPL

Vardo June 1, 2026 2:29 pm

MSEMO wa kuwa adui yako muombee njaa unaonekana bado unaishi, huku mshambuliaji wa JKU, Feisal Hilali maarufu kama ‘Feymar’, akiamini mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) bado hazijaisha.

Akizungumza na Soka la Bongo, Feymar amesema wana matumaini ya kutwaa ubingwa msimu huu, akieleza kuwa anaamini KVZ haitamaliza mechi zake zote zilizobaki bila kupoteza pointi. Amesema kati ya mechi tatu zilizosalia kwa KVZ, anaamini angalau moja utawagharimu na kuwapa nafasi JKU ya kuendelea kupambana kwa ubingwa.

“Mipango yetu ni kuhakikisha tunashinda kila mchezo uliobaki ili kuendelea kumpa presha mpinzani wetu. Tunaamini hawezi kumaliza mechi zote bila kuharibu,” amesema.

Feymar amesema sababu kubwa inayowapa imani ya kuendelea kuwania ubingwa huo, licha ya kuwa nyuma kwa pointi kadhaa, ni ubora wa kikosi walichonacho.

Aliongeza kuwa pamoja na kuwa na kikosi kizuri na benchi bora la ufundi, ushirikiano uliopo kati ya wachezaji na makocha ndiyo nguvu kubwa inayowafanya waendelee kujiamini.

Kwa sasa, msimamo wa ligi unaongozwa na KVZ yenye pointi 58, ikifuatiwa na JKU yenye pointi 52, huku Fufuni ikiwa ya tatu kwa pointi 48.

Mshambuliaji huyo pia aliwataka mashabiki wa JKU kuwa na subira na kuendelea kuiunga mkono timu hiyo, akisisitiza kuwa bado wana nafasi ya kufanya makubwa katika mbio za ubingwa.

MASTAA STARS WAPANIA AFCON 2027 KOCHA UHAMIAJI APATA DAWA ZPL