Taifa Stars

MASTAA STARS WAPANIA AFCON 2027

Vardo June 1, 2026 2:25 pm

WACHEZAJI wa timu ya Tanzania wameonyesha matumaini makubwa ya kikosi hicho katika fainali za Mataifa ya Afrika AFCON, itakayofanyika mwaka 2027, ikihusisha mataifa matatu wenyeji ambao ni Tanzania, Kenya na Uganda.

Wakizungumza na Soka la Bongo katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam yanapofanyika mazoezi ya timu hiyo, wachezaji hao wameonyesha matumaini makubwa kutokana na hamasa kubwa iliyopo, kuanzia serikalini, TFF na wadau wa soka kiujumla.

Akizungumzia suala hilo, kipa wa timu hiyo, Aishi Manula amesema maandalizi bora ya kikosi hicho yanatoa motisha kwa ajili ya Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) ijayo itakayofanyika nchi tatu za Tanzania, Kenya na Uganda.

“Maandalizi tunayofanya yanatoa picha halisi ya kile tunachotakiwa kufanya katika fainali za AFCON 2027, tunatambua ugumu uliopo lakini kwa umoja na ushirikiano wetu naamini tutafanya vizuri zaidi ya miaka ya nyuma tuliyoshiriki,” amesema Manula.

Beki wa kati wa timu hiyo, Bakari Mwamnyeto amesema muitikio mkubwa wa Serikali, TFF na wadau wa soka nchini unatoa matumaini makubwa ya kufanya vizuri, licha ya ushindani kutokana na aina ya timu zenye wachezaji bora na wazoefu.

“Tunachokifanya kwa sasa ni kuonesha namna ambayo tuko tayari kwa ajili ya michuano hiyo mikubwa Barani Afrika, haitokuwa rahisi lakini kuna mwanga mzuri unaonekana, kuanzia sisi wachezaji wenyewe na kile tunachokifanya” amesema Mwamnyeto.

Kwa upande wa beki wa kushoto wa timu hiyo, Nickson Kibabage amesema mechi mbili za kirafiki kati ya Uganda na Rwanda ni sehemu muhimu ya maandalizi kutokana na ubora wa nchi hizo.

“Uganda na Rwanda ni moja ya mataifa tunayojuana nayo vizuri na tumekuwa na ushirikiano katika mambo mbalimbali, naamini itakuwa ni mechi nzuri ambazo zitakuwa ni mojawapo ya maandalizi ya AFCON 2027.

FEI TOTO ACHOMOLEWA STARS, MAJERAHA YATAJWA JKU BADO INA MATUMAINI YA UBINGWA EPL