SIMBA SC YATANGAZWA MABINGWA WPL
HATIMAYE Simba Queens imeipokonya JKT Queens ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake leo baada ya kuitandika Mashujaa Queens mabao 5-2 kwenye mechi ya raundi ya 20 iliyopigwa Uwanja wa KMC Complex.
Simba imetangaza ubingwa leo kabla ya ligi kutamatika zikiwa zimesalia mechi mbili kumalizika msimu wa 2025/26.
Kwenye mechi 20 ilizocheza timu hiyo imeshinda mechi 18 na sare mbili ikiwa haijapoteza mechi yoyote ikikusanya pointi 53 ambazo hazitafikiwa na timu yeyote.
Sare ya 1-1 iliyotoka JKT na Yanga leo imewafanya wananchi hao kukusanya pointi 44 huku wanajeshi hao wakiwa nazo 43.
Ubingwa huo ulikuwa unashikiliwa na JKT Queens ambao msimu huu imeonekana kusuasua na kuwapa nafasi Simba kubeba kwa mara nyingine tena.
Hii inakuwa mara ya tano Simba kubeba taji hilo tangu ligi kuanzishwa mwaka 2016 na Mlandizi Queens kuwa bingwa wa kwanza wa kihistoria.
Kabla ya hapo Simba Queens na JKT Queens zilikuwa zinalingana kwa kubeba mataji timu zote mbili zikibeba mara nne.
Kati ya timu hizo tatu zinazokuwa zinashindania ubingwa kila msimu, Yanga Princess pekee haijawahi kubeba taji hilo tangu timu hiyo ianze kushiriki ligi mwaka 2018.
Taji ililobeba leo linaifanya Simba kukata tiketi ya kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki na Kati kwa Wanawake (CECAFA) ili kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake.
Kwenye michuano hiyo Simba ina rekodi nzuri ya kufika hadi nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2022.
Mwaka 2024 iliporejea tena haikufanya vizuri ikaishia hatua ya makundi ya michuano ya CECAFA.