Habari za michezo

PSG, LUIS ENRIQUE NA REKODI ILIYOTUKUKA ULAYA

Vardo June 1, 2026 12:48 am

BUDAPEST, HUNGURY: PARIS Saint-Germain imeendelea kuthibitisha kuwa ni moja ya timu bora zaidi kuwahi kutokea katika soka la Ulaya baada ya kuwa klabu ya pili pekee kufanikiwa kutetea ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Ushindi wao wa penalti 4-3 dhidi ya Arsenal baada ya sare ya 1-1 katika fainali iliyochezwa Jijini Budapest umeongeza mafanikio yao baada ya ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Inter Milan katika fainali ya mwaka uliopita huko Munich.

Kwa kufanya hivyo, PSG imekuwa timu ya kwanza kutetea taji la Ligi ya Mabingwa tangu Real Madrid iliposhinda mara tatu mfululizo kati ya 2016 na 2018, na klabu ya pili pekee kufanya hivyo katika enzi ya Ligi ya Mabingwa (tangu 1993).

Katika historia yote ya mashindano hayo ya miaka 71, PSG imekuwa klabu ya 10, kushinda taji hilo mara mbili mfululizo.

“Hisia zangu zimechanganyika,” amesema kocha Luis Enrique baada ya mchezo.

“Kuna furaha, uchovu na kila kitu kwa pamoja. Lakini huu ndiyo wakati bora zaidi wa msimu. Bado sisi ni mabingwa, mara mbili mfululizo, jambo la kushangaza sana.”

Wachezaji wote 10 waliokuwa uwanjani walioanza katika ushindi dhidi ya Arsenal pia walikuwepo kwenye kikosi kilichoifunga Inter Milan msimu uliopita.

Tofauti pekee ilikuwa golikipa Matvey Safonov ambaye alichukua nafasi ya Gianluigi Donnarumma aliyesajiliwa na Manchester City majira ya kiangazi yaliyopita.

Katika misimu miwili iliyopita, kikosi cha Luis Enrique kimekuwa na utawala mkubwa katika karibu kila mashindano wanayoshiriki.

Tangu kuanza kwa msimu uliopita, PSG imeshinda mataji nane kati ya 10 yaliyokuwa wanawania, ikikosa tu Kombe la Dunia la Klabu la mwaka jana na Kombe la Ufaransa la msimu huu.

Iwapo itaendelea na ubora huu msimu ujao, PSG inaweza kuwa timu ya tano pekee kushinda Ligi ya Mabingwa au Kombe la Ulaya mara tatu mfululizo.

Hata hivyo, bado ina safari ndefu kufikia rekodi ya Real Madrid ya kushinda Kombe la Ulaya mara tano mfululizo kati ya 1956 na 1960.

“Mwaka huu PSG imeandika historia,” amesema mwandishi wa habari za soka la Ulaya Julien Laurens.

“Msimu uliopita utabaki kuwa wa kipekee, lakini nafikiri wataufurahia zaidi huu kwa sababu walipaswa kupambana kwa nguvu na kurejea kwenye mchezo.

“Msimu uliopita ilikuwa rahisi sana dhidi ya Inter. Kushinda mara mbili mfululizo kunakuweka pamoja na timu bora zaidi kuwahi kutokea.”

MABINGWA WA KIHISTORIA

Paris St-Germain 2025, 2026

Real Madrid 2016, 2017, 2018

AC Milan 1989, 1990

Nottingham Forest 1979, 1980

Liverpool 1977, 1978

Bayern Munich 1974, 1975, 1976

Ajax 1971, 1972, 1973

Inter Milan 1964, 1965

Benfica 1961, 1962

Real Madrid 1956, 1957, 1958, 1959, 1960

MEXICO KUJARIBU SIRAHA ZAKE DHIDI YA AUSTARIA SIMBA SC YATANGAZWA MABINGWA WPL