Geita Gold FC

DAKIKA 90 ZA KIHISTORIA KWA GEITA GOLD KUREJEA LIGI KUU

Vardo June 6, 2026 5:17 pm

ADA ya Geita Gold kudumu katika Ligi ya Championship kwa siku 740, ambazo ni sawa na miaka miwili na siku 10 au miezi 24 na siku 10, hatimaye kikosi hicho kinaweza kurejea Ligi Kuu kesho Jumapili, ikiwa kitashinda dhidi ya Songea United.

Geita inayofundishwa na Kocha, Zubery Katwila ilishuka daraja msimu wa 2023-2024, ambapo ushindi wa kesho dhidi ya timu ya Songea United kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini, Geita, utaifanya kurejea Ligi Kuu Bara, kwani itafikisha pointi 71.

Iko hivi, Geita ndio vinara ikiwa na pointi 68, baada ya kushinda mechi 21, sare tano na kupoteza moja kati ya 27, japo ikiwa itaifunga Songea United itafikisha 71, ambazo zitaihakikishia kupanda rasmi daraja na kucheza Ligi Kuu msimu ujao.

Kwa maana hiyo Geita Gold ikishinda itafikisha pointi 71, ambazo haziwezi kufikiwa na Polisi Tanzania inayoshika nafasi ya tatu na pointi 60, kwani ikishinda mechi zote tatu itaishia 69, kwa sababu zinazopanda moja kwa moja ni timu mbili.

Geita Gold iliyoshuka daraja msimu wa 2023-2024, msimu uliopita wa 2024-2025, wa Championship ilimaliza nafasi ya nne na pointi 56, ikiwa na aliyekuwa Kocha, Mohamed Muya na kushindwa kurejea Ligi Kuu, baada ya kufeli mechi za ‘Play-Off’.

Timu hiyo ilicheza ‘Play-Off’ ya kupanda Ligi Kuu dhidi ya Stand United, ‘Chama la Wana’ iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudiwa ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare nyumbani ya 2-2, kisha kuchapwa ugenini 2-0.

Geita inaingia katika mechi ya kesho na morali kubwa baada ya kutoka kushinda ugenini jijini Mbeya kwa mabao 5-1, dhidi ya KenGold, huku kwa upande wa Songea United ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa wiki iliyopita mabao 2-0 na Kagera Sugar.

Mechi nyingine zitakazopigwa pia zote kesho, Kagera Sugar iliyoichapa Songea United mabao 2-0, itakuwa kwenye Uwanja wa Kaitaba Bukoba kuikaribisha KenGold ya Mbeya, yenye kumbukumbu mbaya baada ya kutoka kuchapwa 5-1, dhidi ya Geita Gold.

Kagera iliyo nafasi ya pili na pointi 65, baada ya kudumu katika Ligi Kuu kwa miaka 20, tangu iliposhiriki mwaka 2005, ilishuka daraja msimu wa 2024-2025, ikishinda mechi tano, sare nane na kupoteza 17, ikishika nafasi ya 15 na pointi 23.

Timu hiyo inayonolewa na aliyekuwa nyota wa Simba, Yanga na timu ya Taifa Stars, Juma Kaseja aliyewahi kuitumikia pia Kagera akiwa mchezaji na kocha wa makipa, ana kazi ya kukipambania kikosi hicho ili kirejee tena katika Ligi Kuu Bara.

Kwenye Uwanja wa Ilulu Lindi, Bigman FC baada ya kutoka sare ya bao 1-1, dhidi ya Stand United, itaikaribisha Gunners FC ya jijini Dodoma, yenye morali kubwa kutokana na wiki iliyopita kuishangaza Mbeya Kwanza ugenini kwa kuichapa mabao 2-1.

Mbeya Kwanza baada ya wiki iliyopita kushindwa kutamba na kuchapwa mabao 2-1, dhidi ya Gunners FC, itakuwa kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora, ikiikaribisha Stand United ‘Chama la Wana’, iliyotoka sare ya bao 1-1 na Bigman FC.

Timu hiyo iliyouzwa katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ikitokea Lindi ilipoweka kambi msimu wa 2024-2025, ilishuka daraja kutokea Ligi Kuu kwenda Championship msimu wa 2021-2022, baada ya kumaliza mkiani mwa nafasi ya 16 na pointi 25.

Msimu huo, Mbeya Kwanza, ilishinda mechi tano tu, sare 10 na kupoteza 15, ikifunga mabao 22 na kuruhusu 39, ikiungana na Biashara United iliyomaliza nafasi ya 15 na pointi 28, hivyo ina kazi kubwa ya kupambana ili kurejea tena Ligi Kuu Bara.

Kwenye Uwanja wa Amani mjini Njombe, Hausung FC inayoburuza mkiani mwa msimamo mwa nafasi ya 16 na pointi tisa, baada ya kutoka sare ya kufungana bao 1-1, dhidi ya Barberian, itaikaribisha Transit Camp iliyotoka suluhu (0-0) mbele ya B19 FC.

Kwa msimu wa 2024-2025, Transit ilimaliza nafasi ya 14 katika Ligi ya Championship na pointi 21, baada ya kushinda mechi tano, sare sita na kupoteza 19, kati ya 30, ilizocheza, ikifunga mabao yake 19 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 50.

Baada ya kumaliza nafasi ya 14, Transit ikacheza mechi mbili za ‘Play-Off’ kusaka tiketi ya kubakia Championship, ambapo ilianza kwa kuitoa Kiluvya United kwa jumla ya mabao 3-2, kisha kuiondosha pia Rhino Rangers ya Tabora kwa jumla ya 4-1.

Kikosi hicho kilipanda rasmi Ligi Kuu msimu wa 2004-2005, kikiwa chini ya Kocha, Stephen Matata ambapo mwaka 2005, timu hiyo ilimaliza nafasi ya tisa na pointi zake 30, ikishinda mechi saba, sare tisa na kupoteza 12, kati ya 28, iliyocheza.

Mwaka 2006, Transit Camp ikashuka daraja kwa kuburuza mkiani mwa timu 16 na pointi 20, baada ya kikosi hicho kushinda mechi tano, sare tano na kupoteza 20, kati ya 30, ambapo kwa sasa inapambana ili kurejea tena katika ufalme wake mpya.

Barberian FC iliyo nafasi ya 15 na pointi 12, baada ya sare ya bao 1-1, dhidi ya Hausung FC, itaikaribisha B19 FC kwenye Uwanja wa Filbert Bayi mkoani Pwani, huku Mbuni ikiwa mwenyeji kwa kukikaribisha kikosi cha maafande wa Polisi Tanzania.

Mbuni inaingia katika mechi hiyo ikiwa na kumbukumbu nzuri baada ya wiki iliyopita kuifunga African Sports ya Tanga bao 1-0, sawa na wapinzani wao Polisi Tanzania inayoshika nafasi ya tatu na pointi 60, iliyoifunga TMA ya Arusha mabao 2-0.

Polisi msimu uliopita wa 2024-2025, haukuwa mzuri sana baada ya kumaliza nafasi ya 10, katika Ligi ya Championship na pointi 33, ikishinda mechi nane, sare tisa na kupoteza 13, ambapo safu ya ushambuliaji ilifunga mabao 44 na kuruhusu 33.

Mechi ya kuhitimisha raundi ya 28 kesho, itapigwa kwenye Uwanja wa Black Rhino jijini, Arusha, ambapo TMA FC iliyochapwa mabao 2-0, dhidi ya Polisi Tanzania, itacheza dhidi ya African Sports ya mjini Tanga, iliyofungwa bao 1-0 na Mbuni FC.

AZERBAIJAN DHIDI YA MALTA KUJIPIMA NGUVU MCHEZO WA KIRAFIKI BILIONEA WA QATAR AIPOTEZEA MAN UNITED