MAGORI AFANYA DHIARA YA KUSHTUKIZA KAMBINI SIMBA, AKUTANA NA BARKER
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi ya Simba SC, Crescentius Magori, amefanya ziara ya kushtukiza katika uwanja wa mazoezi wa timu hiyo na kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Kocha Mkuu, Steve Barker, huku maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu ya NBC yakiendelea kushika kasi.
Ziara hiyo ilifanyika Jumapili, Juni 7, 2026, ambapo Magori alifika kambini kufuatilia maendeleo ya kikosi hicho na kujionea mwenendo wa maandalizi yanayoendelea kuelekea mechi muhimu zijazo.
Katika ziara hiyo, Magori na Barker walionekana wakibadilishana mawazo kwa kina kuhusu hali ya timu, huku pia wakifuatilia kwa karibu mazoezi yaliyowashirikisha wachezaji wa kikosi cha kwanza pamoja na timu ya vijana.
Hatua hiyo inaonyesha dhamira ya uongozi wa Simba kuhakikisha timu inapata mazingira bora ya kufanya maandalizi na kuendelea kuwa katika kiwango kizuri cha ushindani kuelekea hatua za mwisho za msimu.
Ziara ya Magori imekuja wakati Simba ikiendelea na programu maalum ya mazoezi, ikilenga kuboresha utimamu wa wachezaji na kuongeza makali ya kikosi kabla ya mchezo wake ujao.
Wekundu wa Msimbazi wanatarajiwa kuvaana na Pamba Jiji katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC utakaochezwa Juni 14, 2026, kwenye Uwanja wa KMC Complex, mechi ambayo ina umuhimu mkubwa katika harakati zao za kuwania malengo ya msimu huu.
Kwa sasa Simba inaendelea na kambi ya maandalizi kwa ari kubwa, huku benchi la ufundi na viongozi wa klabu wakionyesha mshikamano wa kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri na kuendeleza kasi yake kwenye msimamo wa ligi.