Libasse Gueye Simba SC
Simba SC

CECAFA Kagame Cup: Libasse Gueye Ametua Simba SC, Barker Amsuka Upya Kikosi Kuikabili Jamus FC

Vardo July 27, 2026 12:34 pm

WINGA wa Simba, Libasse Gueye, anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachoshuka dimbani kesho kuikabili Jamus FC ya Sudan Kusini katika mchezo wa pili wa Kundi B wa michuano ya CECAFA Kagame Cup unaoendelea nchini Rwanda.

Gueye, ambaye alichelewa kujiunga na wenzake kambini kutokana na changamoto ya kifamilia, sasa ameungana rasmi na kikosi hicho na kushiriki mazoezi yote kuanzia mwanzo hadi mwisho, ishara kuwa yupo tayari kupewa nafasi katika mchezo huo muhimu.

Kurejea kwa nyota huyo kumempa kocha Steve Barker nafuu kubwa katika kupanga kikosi, kwani kwa sasa wachezaji wote wanaotarajiwa kutumika kwenye mashindano hayo tayari wamewasili Rwanda na wako kwenye maandalizi ya mwisho kuelekea mechi dhidi ya Jamus.

Mbali na mazoezi ya kuimarisha utimamu wa mwili, Barker ametumia pia muda huo kufanyia kazi mbinu na marekebisho ya kikosi, akilenga kuhakikisha Simba inaibuka na ushindi baada ya kuanza kampeni zake kwa sare ya bila kufungana dhidi ya Mogadishu City Club (MCC).

Kocha huyo amesema ameifanyia kazi kasoro zilizojitokeza katika mchezo wa kwanza, akiamini kikosi chake kitaonyesha kiwango bora zaidi dhidi ya Jamus huku ushindani wa namba ukiongezeka kufuatia kurejea kwa Gueye na kukamilika kwa kikosi kizima.

Kwa sasa Simba inaendelea na maandalizi ya msimu mpya sambamba na ushiriki wake katika CECAFA Kagame Cup, huku benchi la ufundi likitarajia kutumia mashindano hayo kukijenga kikosi kitakachoingia kwenye msimu wa 2026/27 kikiwa katika kiwango cha juu.

Mzize Arejea kwa Kasi Yanga: Mbinu Mpya za Mngqithi Kusuka Safu ya Ushambuliaji! Kagoma Awataja Mpanzu, Libasse na Oura Simba SC