Wafungaji Bora Wa Muda Wote Ligi Ya Mabingwa Ulaya (Orodha Mpya)
Kipenga cha Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA Champions League) kimeshapulizwa na mechi za kwanza zimeshashuhudiwa wiki hii. Wakati wanasoka mahiri kama Lamine Yamal, Erling Haaland, Kylian Mbappé, Ousmane Dembélé, na Vinícius Júnior wakisaka kutawala msimu huu, kuna majina ambayo tayari yameshaandika historia isiyofutika katika michuano hii mikubwa duniani.
Hawa hapa ndio wanasoka wanaoongoza kwa kufunga mabao mengi zaidi katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya:
-
Cristiano Ronaldo – Mabao 140
Mreno huyo ndiye mfalme wa mabao wa muda wote katika UEFA Champions League akiwa na mabao 140 katika mechi 183. Alipata mafanikio haya akiwa na Manchester United (21), Real Madrid (105), na Juventus (14). Pia anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi katika msimu mmoja (mabao 17, msimu wa 2013-14).
-
Lionel Messi – Mabao 129
Messi anashika nafasi ya pili, lakini anashikilia rekodi ya kufunga mabao mengi zaidi akiwa na klabu moja — mabao 120 kati ya 129 aliyoyafunga akiwa na Barcelona (mabao 9 akiwa PSG). Pia ndiye mchezaji aliyefunga dhidi ya timu nyingi zaidi tofauti (38) na mwenye rekodi ya kufunga mabao 5 katika mechi moja.
-
Robert Lewandowski – Mabao 109
Mshambuliaji huyo wa Poland alipenya kwenye ukuta wa mabao 100 na sasa ana mabao 109 (akizifungia Borussia Dortmund, Bayern Munich, na Barcelona). Ni mchezaji wa pili katika historia kufikisha angalau mabao 10 au zaidi akiwa na klabu tatu tofauti.
-
Karim Benzema – Mabao 90
Mfaransa huyo aliyepata mafanikio makubwa akiwa Real Madrid na Lyon, amefunga katika misimu 18 mfululizo ya Ligi ya Mabingwa bila kukosa hata msimu mmoja.
-
Raúl González – Mabao 71
Mkongwe wa Real Madrid na Schalke 04, Raúl alikuwa mchezaji wa kwanza katika historia kufikisha mabao 50 kwenye mashindano haya kabla ya rekodi yake kuvunjwa na akina Messi na Ronaldo.
-
Kylian Mbappé – Mabao 71
Mshambuliaji huyo wa Ufaransa anaendelea kupanda kwa kasi. Akiwa amefikisha mabao 50 akiwa na umri mdogo zaidi (miaka 25 na siku 356), Mbappé tayari amesawazisha idadi ya mabao ya mkongwe Raúl na ana nafasi kubwa ya kuingia tatu bora.
-
Erling Haaland – Mabao 59
M mashine huyu wa magoli kutoka Norway ndiye mchezaji aliyefikisha mabao 50 kwa haraka zaidi katika historia ya UEFA Champions League (alitumia mechi 49 pekee).
-
Thomas Müller – Mabao 57
Kiungo mshambuliaji huyu wa Bayern Munich ameweka alama kubwa akitwaa mataji miwili ya UEFA huku akifunga mabao 57 na kutoa pasi za mwisho (assists) 25.
-
Ruud van Nistelrooy – Mabao 56
Mshambuliaji wa zamani wa PSV, Manchester United, na Real Madrid anasalia kuwa mmoja wa wafungaji bora waliowahi kushuhudiwa kwenye historia ya soka la Ulaya.
-
Harry Kane – Mabao 55
Kapteni huyo wa Uingereza amefikisha mabao 50 katika mechi 66 pekee za UEFA Champions League, akiweka wastani sawa na aliotumia Lionel Messi kufikisha idadi hiyo.
-
Thierry Henry – Mabao 50
Mkongwe wa Arsenal, Barcelona, na Monaco anabaki kuwa kinara wa mabao wa Arsenal katika historia ya mashindano haya Ulaya (mabao 35).
-
Mohamed Salah – Mabao 50
Salah aliweka historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kabisa kutoka bara la Afrika kufikisha mabao 50 katika UEFA Champions League.