Ufaransa U-20 Yaipiga Ecuador 3-2 Kombe la Dunia 2026
UFARANSA imeonyesha tinhari na roho ya upambanaji baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Ecuador katika mechi ya Kundi C ya Kombe la Dunia la Wanawake la U-20 (Poland 2026).
Katika mchezo huo uliopigwa juzi, Ufaransa ilikwenda mapumziko ikiwa nyuma kwa mabao 2-1. Hata hivyo, mabeki wake wawili, Aude Bizet na Landryna Lushimba, walibadilisha upepo wa mchezo na kuandika matokeo tofauti kipindi cha pili.
Bizet, ambaye alikuwa nahodha na kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa Mechi (Player of the Match), alisawazisha bao hilo dakika ya 48 kwa kichwa safi akimalizia mpira wa adhabu uliopigwa na Juliane Denizot.
Lushimba alitimsha msumari wa mwisho dakika ya 87 baada ya kufunga bao la ushindi kupitia mpira wa kona uliopigwa na Ornella Graziani, ushindi uliowapa Wafaransa pointi tatu muhimu.
Akizungumza baada ya mechi, Lushimba alisema ushindi huo ulikuwa wa ushirikiano wa timu nzima:
“Nilimshukuru Mungu kwa sababu nilihisi bao likija litaturudisha mchezoni. Tulibaki pamoja na huu ulikuwa ushindi wa timu. Sikuwa mimi peke yangu, kila mmoja alifanya kazi kubwa.”
Kwa upande wake Bizet alisisitiza kuwa mechi hiyo imewajenga kisaikolojia, ingawa walikosa kutumia vizuri baadhi ya nafasi:
“Tumepata ugumu kumalizia nafasi zetu, lakini michezo ya aina hii inatufanya kuwa imara zaidi na tutakuwa tayari kwa mchezo unaofuata.”
Kocha Philippe Joly alieleza kuwa alilazimika kubadili mbinu baada ya kuona sare haitawatosha, ikizingatiwa walitoka sare ya 1-1 dhidi ya Korea Kusini katika mchezo wa kwanza. Joly aliwaingiza Lina Gay na Celia Chabod kipindi cha pili kuongeza nguvu ya mashambulizi.
“Tulibadilisha mambo kidogo na wasichana waliitikia vizuri. Kuna njaa kubwa ya ushindi ndani ya kundi hili na roho yao ya pamoja ilikuwa ya kupigiwa mfano,” alisema Joly.
Ushindi huo umedhihirisha pia kuwa Ufaransa ni hatari kwenye mipira iliyokufa (set-pieces), kwani mabao yote mawili ya kipindi cha pili yalipatikana kupitia mpira wa adhabu na kona.