Simba SC

BAJABER AFANYA MAAJABU KENYA, SIMBA YABAKI KWENYE MTEGO

Vardo June 8, 2026 9:03 am

MSHAMBULIAJI wa Simba SC, Mohammed Bajaber, ameendelea kuonyesha ubora wake akiwa na kikosi cha Taifa cha Kenya, jambo linalozidi kuibua maswali ndani ya klabu hiyo kuhusu hatma yake kuelekea msimu ujao.

Bajaber kwa sasa yuko kwenye majukumu ya timu ya taifa ya Kenya (Harambee Stars), ambayo jana ilicheza mechi ya kirafiki ya kimataifa katika kalenda ya FIFA na kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Lesotho.

Katika mchezo huo, Bajaber alikuwa miongoni mwa nyota waliowika zaidi baada ya kuhusika moja kwa moja katika mabao manne ya timu yake.

Mshambuliaji huyo alifunga mabao mawili na pia alichangia upatikanaji wa mabao mingine, akionyesha kiwango bora kilichowavutia wengi.

Kiwango hicho kimezidi kuipa Simba kazi ngumu ya kufanya maamuzi kuhusu mustakabali wa mchezaji huyo, wakati kukiwa na taarifa kwamba klabu hiyo ilikuwa inapitia upya nafasi yake ndani ya kikosi kuelekea dirisha la usajili la msimu mpya.

Licha ya kuonyesha uwezo mkubwa akiwa na timu ya taifa, Bajaber ameshindwa kupata mwendelezo wa kucheza ndani ya Simba kutokana na kusumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara yaliyomuweka nje kwa vipindi tofauti vya msimu.

Hali hiyo ilimfanya ashindwe kupata nafasi ya kutosha chini ya benchi la ufundi, jambo lililochangia kushuka kwa mchango wake ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi katika mashindano mbalimbali.

Hata hivyo, kiwango alichoonyesha akiwa na Kenya kinaweza kubadili mtazamo wa viongozi na benchi la ufundi la Simba, ambao sasa wanakabiliwa na uamuzi mgumu wa kuamua kama waendelee kuwa na mshambuliaji huyo au waachane naye mwishoni mwa msimu.

EVALISTO AKIRI UGUMU MISRI