EVALISTO AKIRI UGUMU MISRI
KIUNGO mshambuliaji wa Mtanzania anayekipiga Fouad FC ya Misri, Oscar Evalisto, amesema msimu uliomalizika haukuwa wa mzuri kwake baada ya kushindwa kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara tangu alipojiunga na klabu hiyo akitokea Makadi FC, timu inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu nchini humo.
Oscar amekiri kuwa ushindani mkubwa ndani ya kikosi umemfanya ashindwe kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza hali iliyochangia kushindwa kufikia malengo aliyojiwekea mwanzoni mwa msimu.
Akizungumza na Soka la Bongo Evalisto amesema “Kwa upande wangu haujawa msimu mzuri. Tangu nijiunge na timu hii nimekuwa nikikutana na changamoto ya kupata nafasi ya kuanza mara kwa mara hilo limeathiri kiwango changu,” amesema.
Katika msimu wa 2025/26, Oscar amefanikiwa kufunga mabao matatu na kutoa assist moja, takwimu ambazo amesema hazimridhishi kutokana na uwezo alionao na matarajio aliyokuwa nayo wakati anajiunga na klabu hiyo.
“Mabao matatu na assist moja si takwimu nzuri kwangu. Ninaamini nina uwezo wa kufanya zaidi ya hapo, najipanga vizuri ili msimu ujao niwe na mchango na kuanza kikosi cha kwanza,” ameongeza.
“Mpira unahitaji uvumilivu na kujituma. Ninaamini muda wangu utafika, na msimu ujao nataka kuonyesha uwezo wangu kwa kufunga mabao mengi na kutengeneza nafasi zaidi za kufunga,” amesema.
Kabla ya kuzitumikia timu za Misri Evalisto aliwahi kukupiga Mlandege.