Michezo

DAR LEOPARDS KUKIWASHA TAMASHA LA RAGA

Vardo June 10, 2026 11:24 pm

IKIWA zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa Tamasha la Touch Rugby Tournament, waandaaji wa mashindano hayo, Dar Leopards RFC wamewaomba mashabiki wa michezo huo kujitokeza kwa wingi kwenye Uwanja wa Ufundi, Mikocheni ulioko Jijini Dar es Salaam.

Mashindano hayo yanayotarajiwa kuzikutanisha timu 20 kutoka maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki yatafanyika Jumamosi, Juni 13 kuanzia asubuhi hadi jioni, huku ushindani mkubwa ukitarajiwa kutoka kwa timu zinazowania kumng’oa bingwa mtetezi Karen Crusaders.

Mbali na ubingwa wa jumla, waandaaji wametangaza zawadi maalumu zitakazoongeza hamasa kwa washiriki. Kutakuwa na tuzo za mchezaji bora wa kiume, mchezaji bora wa kike, mchezaji bora wa vijana pamoja na mkongwe bora wa mashindano hayo.

Katika kuongeza upekee wa tukio hilo, washindi watatunukiwa medali za kipekee zilizotengenezwa kwa ubunifu wa sanaa ya Tingatinga, hatua inayolenga kuonyesha utambulisho wa Kitanzania sambamba na kuenzi mchango wa sanaa katika michezo.

Mmoja wa viongozi wa Dar Leopards, Victoria Beach ameeleza kuwa kila kitu kipo tayari kwa ajili ya siku hiyo huku ukisisitiza kuwa tamasha hilo si kwa wachezaji pekee bali pia kwa familia na wadau wa michezo wanaotaka kupata burudani ya mwisho wa wiki.

YANGA, SIMBA, TRA UNITED ZIMEKULA KIBANO CHA TPLB BURUDANI, BAHATI NA USHINDI NDANI YA GATES OF LOVE