Peter Shalulile Aandika Ujumbe wa Machozi Mamelodi Sundowns Baada ya Kusajiliwa Yanga
DAR ES SALAAM, Tanzania — Mshambuliaji wa kimataifa kutoka nchini Namibia, Peter Shalulile, ameaga rasmi klabu yake ya zamani ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, muda mfupi baada ya kutangazwa rasmi kama mchezaji mpya wa mabingwa wa Tanzania, Yanga SC.
Shalulile, ambaye ameweka rekodi na historia kubwa nchini Afrika Kusini, ametumia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii kutoa salamu za shukrani za dhati kwa viongozi, benchi la ufundi, wachezaji wenzake pamoja na mashabiki wa “Masandawana”.
Kuvaa Jezi ya Sundowns Ilikuwa Heshima Kubwa
Katika ujumbe wake, nyota huyo alieleza kuwa kuchezea Mamelodi Sundowns ilikuwa ni miongoni mwa mafanikio na heshima kubwa zaidi kwenye taaluma yake ya soka, akisisitiza kuwa mafanikio yake yote yalitokana na ushirikiano wa kitimu.
“Kila bao nililofunga, kila shangwe niliyoshiriki na kila taji nililoinua lilitokana na nguvu ya pamoja. Ninaondoka nikiwa na kumbukumbu zisizosahaulika, shukrani za dhati na upendo mkubwa kwa klabu hii ya ajabu. Mamelodi Sundowns itaendelea kuwa na nafasi ya kipekee moyoni mwangu,” aliandika Shalulile.
Mshambuliaji huyo alimalizia kwa kuwashukuru mashabiki kwa sapoti yao isiyoyumba kwa kusema: “Mara moja ukiwa wa Njano, utabaki sehemu ya familia milele.”
Kutua Yanga Kuongoza Safu ya Ushambuliaji
Baada ya kufunga rasmi ukurasa wake na mabingwa hao wa Afrika Kusini, Shalulile sasa anatarajiwa kutua nchini muda wowote kuanzia sasa kujiunga na kikosi cha Wananchi.
Usajili huu unakuja kama ingizo jipya lenye uzito mkubwa katika kuelekea maandalizi ya msimu wa 2026/27, ambapo Shalulile anatarajiwa kuwa nguzo kuu katika safu ya ushambuliaji ya Yanga SC kwenye Ligi Kuu ya NBC na michuano ya kimataifa ya CAF.