Singida Big Stars FC

ELVIS RUPIA KUACHANA NA SINGIDA BS KUNUKIA KENYA

Vardo June 10, 2026 8:32 am

MSHAMBULIAJI mahiri wa Singida Black Stars, Mkenya Elvis Rupia yuko katika mazungumzo ya kurejea katika timu ya Kenya Police FC ya kwao Kenya aliyowahi kuichezea awali, baada ya klabu hiyo kuanza kumuwania kwa ajili ya kuongezea nguvu.

Taarifa kutoka Kenya, zinaeleza Rupia yupo katika mazungumzo na Kenya Police FC inayomuhitaji kumrejesha tena, japo kwa sasa timu hiyo itakabiliwa na upinzani mkubwa kutoka kwa wapinzani wao, baada ya AFC Leopards ya Kenya pia kumuhitaji.

Sababu za Kenya Police FC kuweka nguvu zaidi ya kumrejesha mshambuliaji huyo, ni baada ya nyota wa kikosi hicho, Yves Koutiama raia wa Burkina Faso aliyeifungia mabao 10 ya Ligi Kuu ya Kenya msimu wa 2025-2026, kudaiwa anajiunga na Yanga.

Koutiama aliyejiunga na Kenya Police FC, tangu Januari 4, 2026, akitokea USFA Ouagadougou ya kwao Burkina Faso, inadaiwa yupo hatua za mwisho za kujiunga na Yanga, ambayo imeonyesha nia ya kumuhitaji kutokana na kiwango chake bora kwa sasa.

Rupia alijiunga na Singida kwa msimu wa 2023-2024, akitokea Police FC ya kwao Kenya na alifunga mabao 27 na kuivunja rekodi iliyochukua miaka 47, katika Ligi Kuu ya Kenya ya Moris Aloo Sonyi aliyefunga 26, mwaka 1976, akiwa na Gor Mahia.

Katika msimu wake wa kwanza, Rupia alichezea timu mbili tofauti akianza Singida Fountain Gate kisha dirisha dogo akatua Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars na kwa msimu mzima alifunga jumla ya mabao sita akiwa na klabu zote mbili.

Katika misimu yote tangu atue nchini, msimu bora kwake ni wa 2024-2025, katika Ligi Kuu Bara kutokana na idadi kubwa ya mabao aliyofunga, ambapo kiujumla alichangia 12, baada ya kufunga 10 na kuasisti mawili kati ya 45, ya timu hiyo nzima.

Hata hivyo, msimu huu wa 2025-2026 umekuwa ni wa tofauti kwake, kwani amefunga mabao matatu hadi sasa ya Ligi Kuu Bara, huku bao la mwisho kufunga ni la sare ya timu hiyo ya 1-1, dhidi ya kikosi cha maafande wa Mashujaa FC, Aprili 16, 2026.

JINA LA MSENEGAL MEZANI KWA IBENGE BARKER ATABIRI MAKUBWA KWA MBEGU NA VEDASTUS SIMBA