BARKER ATABIRI MAKUBWA KWA MBEGU NA VEDASTUS SIMBA
KOCHA Mkuu wa Simba, Steve Barker, amesema mabeki vijana Hussein Mbegu na Vedastus ni miongoni mwa wachezaji wenye mustakabali mkubwa ndani ya klabu hiyo kutokana na uwezo wao wa kujifunza haraka na kuendelea kukua kwa kasi katika mchezo.
Barker amewapongeza vijana hao ambao walipandishwa kutoka timu ya vijana na kupewa nafasi katika kikosi cha wakubwa, akieleza kuwa wameonyesha maendeleo makubwa na kuendelea kutumia vyema nafasi wanazopewa katika timu ya kwanza.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini amesema kila wanapopata nafasi ya kucheza, Mbegu na Vedastus huonyesha kiwango kizuri pamoja na utayari wa kujifunza, jambo linalowapa nafasi kubwa ya kuwa sehemu muhimu ya Simba katika siku zijazo.
Akizungumzia mafanikio ya safu ya ulinzi ya timu hiyo, Barker amesema hayategemei uwezo wa mchezaji mmoja mmoja pekee, bali yanatokana na ushirikiano na uelewa wa majukumu kwa kila mchezaji ndani ya kikosi.
“Mafanikio ya safu ya ulinzi ya Simba hayatokani na mchezaji mmoja mmoja pekee, bali yanachangiwa na uelewa wa majukumu kwa kila mchezaji ndani ya kikosi. Kila mchezaji anatambua wajibu wake akiwa uwanjani au benchi,” amesema Barker.
Ameeleza kuwa katika mazoezi ya kila siku, wachezaji wote hupewa majukumu maalumu na kufundishwa namna ya kucheza timu inapokuwa na mpira pamoja na jinsi ya kujilinda dhidi ya mashambulizi ya wapinzani.
Barker ameongeza kuwa uwepo wa mabeki wenye uzoefu kama Rushine De Reuck na Ismael Touré umekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya Mbegu na Vedastus, kwani wanawapa mwongozo na kuwasaidia kujifunza mahitaji ya soka la ushindani wa juu.
Kocha huyo amesema ana matumaini ya kuwaona mabeki wengine wa kikosi hicho, akiwemo Wilson Nangu na Abdulrazq Hamza, wakirejea kwa nguvu baada ya kupitia changamoto mbalimbali na kuendelea kupigania nafasi zao ndani ya timu.
Kwa mujibu wa Barker, ushindani wa ndani ya kikosi ni jambo muhimu katika maendeleo ya timu kwa kuwa unaleta uwiano mzuri kati ya uzoefu wa wachezaji wakubwa na nguvu pamoja na ari ya vijana wanaochipukia, hali ambayo ndiyo msingi wa kuijenga Simba imara kwa sasa na katika miaka ijayo.