Singida Big Stars FC

PAMBA JIJI YAPIGWA PIGO, AELEKEA SINGIDA BLACK STARS

Vardo June 10, 2026 8:41 am

UONGOZI wa Singida Black Stars upo katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa kipa wa Pamba Jiji FC, Yona Amosi, baada ya nyota huyo kuamua kutoongeza mkataba wake na klabu hiyo.

Taarifa kutoka ndani ya Singida Black Stars zinaeleza kuwa mazungumzo kati ya pande hizo mbili yamefikia hatua nzuri, huku klabu hiyo ikionekana kuwa na nafasi kubwa ya kunasa saini ya kipa huyo kuelekea msimu ujao.

Amosi amedhamiria kuondoka Pamba Jiji mara tu mkataba wake utakapomalizika, jambo ambalo limeifanya Singida Black Stars kuharakisha mipango yake ya kuhakikisha inampata mlinda mlango huyo mwenye uzoefu mkubwa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa chanzo cha habari kilicho karibu na mchezaji huyo, Amosi tayari ameonyesha nia ya kujiunga na Singida Black Stars licha ya kuwepo kwa taarifa zinazomhusisha na Simba.

Chanzo hicho kilieleza kuwa hadi sasa Simba haijawasilisha ofa rasmi kwa kipa huyo, hali iliyompa nafasi ya kufanya maamuzi yake mapema kuhusu mustakabali wake wa soka.

“Masuala ya Simba yalibaki kuwa tetesi tu kwa sababu hakuna ofa rasmi iliyowasilishwa. Singida walionesha nia ya dhati na ndiyo maana Amosi ameona ni vyema kujiunga nao kwa msimu ujao,” kilisema chanzo hicho.

Amosi amekuwa miongoni mwa makipa waliovutia zaidi katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kutokana na kiwango chake bora langoni.

Uamuzi wake wa kuondoka Pamba Jiji umefungua milango kwa klabu mbalimbali kuwania huduma yake, lakini kwa sasa Singida Black Stars ndiyo inaonekana kuwa karibu zaidi kumnasa.

BARKER ATABIRI MAKUBWA KWA MBEGU NA VEDASTUS SIMBA USAJILI WA KISHINDO, SIMBA YAMTAKA SHUJAA WA NIGERIA AFCON