Simba SC

USAJILI WA KISHINDO, SIMBA YAMTAKA SHUJAA WA NIGERIA AFCON

Vardo June 10, 2026 8:45 am

KATIKA kuimarisha safu ya ulinzi kuelekea msimu wa 2026/27, uongozi wa Simba umeanza mazungumzo ya kina kwa ajili ya kumsajili kipa wa kimataifa wa Nigeria, Stanley Nwabali, ambaye anatajwa kuwa miongoni mwa walinda mlango wanaowindwa kwa karibu na mabosi wa Wekundu wa Msimbazi.

Taarifa zilizopatikana zinaeleza kuwa Simba inamwona Nwabali kama mbadala sahihi wa Moussa Camara, ambaye mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwishoni mwa msimu huu huku akiwa hajaonyesha nia ya kuendelea kubaki klabuni hapo.

Imeelezwa kuwa iwapo usajili wa Nwabali utakamilika, kutakuwa na mabadiliko katika nafasi ya makipa wa kigeni ndani ya kikosi hicho. Kwa mujibu wa kanuni za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), haitaruhusiwa kuwa na makipa wawili wa kigeni, jambo ambalo linaweza kumlazimu Djibrilla Kasali kupisha nafasi hiyo.

Chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kimeeleza kuwa Simba imeandaa ofa ya mshahara wa Dola za Marekani 12,000 kwa mwezi, sawa na zaidi ya Sh milioni 31 za Kitanzania, pamoja na bonasi mbalimbali ili kumshawishi kipa huyo kusaini mkataba wa kuitumikia timu hiyo msimu ujao.

Kwa sasa, Nwabali ni mchezaji huru baada ya kuachana na Chippa United ya Afrika Kusini. Hali hiyo imeifanya Simba kuona fursa nzuri ya kuingia kwenye mbio za kuwania saini yake huku ikikabiliana na ushindani kutoka klabu nyingine zinazomhitaji nyota huyo.

Kipa huyo alipata umaarufu mkubwa kutokana na kiwango chake bora akiwa na timu ya taifa ya Nigeria, Super Eagles, hasa katika mashindano makubwa ya kimataifa ambapo alitoa mchango mkubwa na kuvutia macho ya wadau wengi wa soka barani Afrika.

“Uongozi wa Simba unaamini kuwa usajili wa Nwabali utaongeza ushindani katika nafasi ya golikipa na kuipa timu uimara zaidi katika mashindano ya ndani na ya kimataifa,” kilisema chanzo hicho.

Wakati huo huo, Simba inaendelea na mchakato wa kuunda kikosi imara kitakachokuwa na uwezo wa kupambana kwa mafanikio katika mashindano mbalimbali msimu ujao.

Hivi karibuni, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, Crestius Magori, alisema kuwa masuala yote ya usajili yapo mikononi mwa Kocha Mkuu Steve Barker, ambaye ana jukumu la kuamua ni wachezaji gani watasajiliwa na ni nani ataachwa ili kuimarisha kikosi

PAMBA JIJI YAPIGWA PIGO, AELEKEA SINGIDA BLACK STARS