JULIO ATAMBA ASEMA ANAIJUA YANGA KULIKO WENGI
KOCHA Mkuu wa Mashujaa FC, Jamhuri Kihwelo ‘Julio’, amesema hana presha yoyote kuelekea mchezo dhidi ya Yanga, akieleza kuwa historia yake dhidi ya mabingwa hao wa Tanzania Bara inampa imani kubwa ya kupata matokeo mazuri.
Mashujaa FC wanatarajiwa kuwakaribisha Yanga Juni 13, 2026, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaopigwa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, huku timu zote zikiwania matokeo muhimu katika hatua za mwisho za msimu..
Julio amesema katika maisha yake ya ukocha amekuwa na rekodi nzuri dhidi ya Yanga akiwa na timu mbalimbali alizowahi kuzifundisha, jambo linalomfanya kuingia kwenye mchezo huo akiwa na kujiamini zaidi.
Kocha huyo alidai kuwa amewahi kupata ushindi dhidi ya Yanga alipokuwa akiifundisha Simba, Kagera Sugar na Mwadui FC, huku akisisitiza kuwa anaelewa vyema ubora na mapungufu ya wapinzani wake.
Akizungumzia kikosi cha Yanga, Julio amesema anakiheshimu, lakini haoni sababu ya kuwa na hofu nacho.
Amemtaja Prince Dube kuwa ni mshambuliaji anayejua kutumia nafasi zinazotengenezwa na wenzake, huku akisema Pacome Zouzoua ana uwezo mkubwa wa kulisukuma na kulimiliki vizuri soka.
Pia alimzungumzia Mudathir Yahya akisema ni mchezaji mwenye akili nyingi uwanjani, lakini anaamini kuwa akiwawekea wachezaji wa kumdhibiti pamoja na nyota wengine muhimu wa Yanga, timu hiyo inaweza kuzuiwa kucheza kwa ubora wake wa kawaida.
“Yanga wanajua kabisa wanakwenda kucheza dhidi ya kocha anayejiamini sana. Nilivyokuwa najiamini nilipokuwa Simba ndivyo ninavyojiamini sasa nikiwa Mashujaa. Nakumbuka mara nyingi nilizowafunga, lakini sikumbuki mara ya mwisho wao kunifunga. Ninaamini tutapata alama muhimu katika mchezo huu,” amesema Julio.