Wema Sepetu Afunguka Siku 40 ya Mwanae na Ugonjwa
Baada ya siku kadhaa za sintofahamu na maswali mengi kutoka kwa mashabiki kuhusu kutofanyika kwa sherehe ya siku 40 ya mtoto wake wa kiume, staa wa filamu nchini Tanzania, Wema Sepetu, hatimaye amevunja ukimya na kuweka wazi kilichojiri nyuma ya pazia.
Kupitia Instagram Story yake leo, Wema amewatolea uvivu watu waliokuwa wakihoji kwa kejeli kuhusu sherehe hiyo, akidai wamekuwa wakitafuta makosa tangu alipofanya ibada ya Aqiyqah ya mwanae.
“Haya nyie waja mnaodai 40 mtasema mtoto wa kwenu… Mbona kama mapovu yanawatoka sana… Mmenikosa kosa kwenye Aqiyqah ndo mlitaka kuja kunimaliza sio… Mnikome…!!!” alindika Wema, kisha kuongeza: “Sasa mkae kwa kutulia… EBO…!!!”
Changamoto za Afya na Kulazwa Hospitalini
Mbali na kuwajibu wakosoaji wake, Wema alikiri kuwa amekuwa akipitia kipindi kigumu cha kiafya kilichomfanya ahofie hata maisha yake.
Alifichua kuwa mara tu baada ya kumaliza Aqiyqah ya mwanae, alianza kuugua ghafla magonjwa yasiyoeleweka yaliyosababisha alazwe hospitalini na kuwekewa dripu kwa siku kadhaa.
“Nimeumwa magonjwa ya ajabu ajabu… Nikajua nakufa… Nimelazwa baada ya Aqiqah tu ya mtoto since last Monday,” alieleza Wema huku akiamatanisha picha inayomwonyesha akiwa kitandani hospitalini.
Kilichokwamisha Sherehe ya Siku 40
Siku ya 40 ya mtoto wa Wema ilipangwa kufanyika Julai 23, 2026, katika ukumbi wa SuperDome, Masaki jijini Dar es Salaam, ambapo awali alitangaza viingilio vilivyozua mjadala mkubwa mtandaoni.
Hata hivyo, siku hiyo ilipowadia hakukufanyika sherehe wala kutolewa maelezo yoyote rasmi, jambo lililozua maswali mengi. Maelezo ya leo yanamaliza utata huo, ikionekana wazi kuwa changamoto za afya ndizo zilizovuruga mipango yote.
Wema Sepetu alijifungua mtoto wake wa kwanza wa kiume Juni 12, 2026, tukio lililopokelewa kwa furaha kubwa baada ya miaka mingi ya kusubiri. Hivi sasa, mashabiki na wadau wa burudani wanaendelea kumtumia jumbe za kumtakia afya njema na kupona haraka.