Kocha Ben Lee Tanzania
Michezo Bongo

Kocha Ben Lee Kutoka Marekani Kutoa Mafunzo ya Uogelea Dar

Vardo July 28, 2026 4:39 pm

Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limesema ujio wa kocha wa kimataifa wa mchezo wa kuogelea kutoka Marekani, Ben Lee, ni fursa ya dhahabu kwa makocha na waogeleaji wazawa kujifunza mbinu za kisasa za viwango vya kimataifa.

Kocha Lee, ambaye ana uzoefu mkubwa wa kufundisha katika ngazi za NCAA na Michezo ya Olimpiki, ataongoza programu maalumu ya wiki tatu ya kuendeleza mchezo huo katika Shule ya Kimataifa ya Monti, iliyopo Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa mapokezi ya kocha huyo, Afisa Michezo wa BMT, Petro Gallos, amewataka wakufunzi wa ndani kutumia vyema fursa hiyo kwa kuchota ujuzi utakaosaidia kuinua mchezo wa kuogelea nchini.

Naye Mkurugenzi wa Ufundi wa Chama cha Uogeleaji Tanzania (TSA), Amina Mfaume, alieleza kuwa mafunzo hayo yataongeza ufanisi mkubwa kwa makocha wa ndani na kutoa mwongozo wa jinsi ya kuandaa waogeleaji wanaoshindana katika viwango vya kimataifa.

Maandalizi ya Mashindano ya CANA Zone 3

Mkurugenzi wa Shule ya Kimataifa ya Monti, Fatma Fernandez, alisema ujio wa Kocha Lee umekuja wakati muafaka ambapo Tanzania inajiandaa na mashindano mbalimbali, yakiwemo ya CANA Zone 3 yanayotarajiwa kushirikisha zaidi ya waogeleaji 40 wa Kitanzania.

“Lengo letu si tu kuandaa waogeleaji kwa ajili ya mashindano ya sasa, bali ni kujenga mfumo endelevu wa muda mrefu utakaowezesha Tanzania kuzalisha wanamichezo wenye uwezo wa kushindana kimataifa,” alisema Fernandez.

Ratiba na Utaratibu wa Mafunzo

Programu hiyo imegawanywa katika maeneo matatu: makocha, waogeleaji, na wazazi.

  • Mafunzo ya Makocha: Yatafanyika kuanzia Julai 28 hadi Julai 30, 2026.

  • Kambi ya Waogeleaji: Yataendelea kwa makundi mbalimbali ya umri na kuhitimishwa Agosti 14, 2026.

  • Muda na Eneo: Mafunzo yanafanyika kila siku kuanzia saa 2:00 asubuhi hadi saa 5:00 asubuhi katika bwawa la kisasa la Shule ya Kimataifa ya Monti, Mikocheni.

Fernandez alibainisha kuwa mafunzo hayo yanatolewa bure kwa makocha wote waliosajiliwa na TSA, huku gharama zote za kumleta Kocha Lee zikiwa zimebebwa na Shule ya Monti.

Kwa upande wake, Kocha Ben Lee, ambaye pia ni mwanzilishi wa taasisi ya RaceBetter, alishukuru kwa mapokezi na kueleza kuwa yupo tayari kushirikiana na wadau wa Tanzania kuweka misingi thabiti ya mafanikio ya muda mrefu.

Wema Sepetu Afunguka Siku 40 ya Mwanae na Ugonjwa