Rayon Sports CECAFA Kagame Cup
Habari za michezo

Rayoon Sports Waanza CECAFA Kagame CUP 2026 Kwa Kishindo.

Vardo July 28, 2026 3:58 pm

Kama ilivyo nchini Tanzania ambapo huwezi kutaja ushindani wa soka bila kuzungumzia miamba ya Simba na Yanga, ndivyo ilivyo pia nchini Rwanda kati ya vigogo APR na Rayon Sports. Ushindani huo wa jadi ulijidhihirisha tena juzi Jumapili kwenye Uwanja wa Amahoro, Kigali.

Rayon Sports ilifanikiwa kuondoka na ushindi mnono wa mabao 2-0 dhidi ya KVZ ya Zanzibar, katika mchezo wa Kundi C wa Kombe la CECAFA Kagame Cup 2026. Ushindi huo uliwapa fursa kubwa mashabiki wa Rayon kuwakejeli wapinzani wao wakubwa, APR, ambao walianza mashindano hayo kwa kupokea kichapo kizito cha mabao 5-0 kutoka kwa Gor Mahia ya Kenya.

Mambo Yabadilika Kipindi cha Pili

Katika kipindi cha kwanza, KVZ walisimama kidete na kufanikiwa kuzima mashambulizi yote ya Rayon Sports, hali iliyofanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa suluhu ya 0-0 licha ya presha kubwa kutoka kwa wenyeji.

Hata hivyo, mambo yalibadilika katika kipindi cha pili baada ya Rayon kuongeza kasi na mbinu mpya za ushambuliaji:

  • Dk 69: Junior Kameni aliifungia Rayon bao la kwanza kwa njia ya penalti na kuamsha shangwe za kukata na shoka uwanjani.

  • Dk 82: Daniel Muhoza aligongelea msumari wa pili na kuhitimisha matumaini ya KVZ kurejea mchezoni.

Matokeo hayo yaliipa Rayon Sports pointi tatu muhimu katika mbio za kutinga hatua ya nusu fainali, huku ikiwaweka nafasi nzuri ikilinganishwa na APR.


‘Viking Clap’ Yatisa Uwanja wa Amahoro

Mbali na matokeo ya uwanjani, mashabiki wa Rayon Sports waliteka hisia za wengi kwa mtindo wao wa kipekee wa ushangiliaji maarufu kama ‘Viking Clap’.

Kabla ya mpira kuanza, maelfu ya mashabiki waliinua shamrashamra kwa kusubiri ngoma ipigwe mara mbili, kisha kupiga makofi kwa mpangilio huku wakipaza sauti “Huu…!” kwa pamoja. Mtindo huo ulitengeneza mazingira ya kipekee na ya kuvutia hata kwa mashabiki wa timu pinzani, ukiimarisha hamasa na umoja uwanjani.

Baada ya filimbi ya mwisho, uwanja mzima ulilipuka kwa nyimbo na vijembe dhidi ya APR, ukithibitisha kuwa ushindani wa timu hizo mbili una sura sawa na dabi ya Kariakoo—ambapo furaha ya mmoja ni simanzi na kejeli kwa mwingine!

Kocha KVZ Ashusha Presha: “Nyasi Bandia Zitawatoa Al Hilal Kagame Cup” Kocha Ben Lee Kutoka Marekani Kutoa Mafunzo ya Uogelea Dar