Hababuu Omar KVZ
Michezo Bongo

Kocha KVZ Ashusha Presha: “Nyasi Bandia Zitawatoa Al Hilal Kagame Cup”

Vardo July 28, 2026 3:47 pm

KOCHA Mkuu wa KVZ ya Zanzibar, Hababuu Omar, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo na kusisitiza kuwa hana wasiwasi wowote kuelekea pambano lao linalofuata dhidi ya miamba ya Sudan, Al Hilal, katika Mshindano ya Kombe la CECAFA Kagame 2026.

Hababuu anaamini kuwa kuchezwa kwa mchezo huo kwenye Uwanja wa Kigali Pele wenye nyasi bandia kutawapa faida kubwa ya kiufundi ukilinganisha na wapinzani wao.

Kwa mujibu wa kocha huyo, asilimia kubwa ya viwanja vinavyotumika kwenye Ligi Kuu ya Zanzibar (ZPL) ni vya nyasi bandia, jambo linalowafanya wachezaji wake kuwa wazoefu na huru zaidi wanapocheza kwenye uso huo wa uwanja.

“Nafikiri tutakuwa na nafasi nzuri sana ya kucheza soka letu la kawaida. Wachezaji wetu wamezoea zaidi kucheza kwenye nyasi bandia, hivyo naamini wataonyesha kiwango bora zaidi kuliko mchezo uliopita,” alisema Hababuu.

Kurejea Baada ya Kipigo cha Rayon Sports

KVZ ilianza vibaya michuano hiyo baada ya kukubali kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya wenyeji Rayon Sports katika Uwanja wa Amahoro—matokeo yaliyowaacha bila pointi mkononi.

Akizungumzia mchezo huo wa kwanza, Hababuu alieleza kuwa presha ya mashabiki wengi wa Rayon Sports na ukweli kwamba kikosi chake kina wachezaji wengi wapya ilichangia kwa kiasi kikubwa kushindwa kutulia.

“Ilikuwa mechi ngumu kutokana na mazingira na sapoti kubwa waliyokuwa nayo wenyeji. Pia tuna wachezaji wengi wapya ambao bado wanazoeana, lakini nina imani kwenye mchezo ujao watakuwa watulivu zaidi uwanjani,” aliongeza.

Kibarua Dhidi ya Al Hilal (Julai 29)

KVZ itashuka dimbani Julai 29, 2026 kuwakabili Al Hilal katika mchezo ambao unachukuliwa kama wa ‘kufa au kupona’ ili kufufua matumaini yao ya kutinga hatua ya mtoano. Kocha Hababuu amesisitiza kuwa kikosi chake kiko tayari kupambana mpaka mwisho na hawajakata tamaa.

CECAFA Kagame Cup 2026: Simba na Singida Black Stars Kusaka Ushindi wa Kwanza Leo Kigali