Simba SC

BAJABER AAHIDI MAKUBWA SIMBA BAADA YA KUPONA MAJERAHA

Vardo June 10, 2026 3:28 pm

MSHAMBULIAJI wa Simba, Mohammed Bajaber, amesema bado hajafikia kiwango chake bora licha ya kuanza kurejea uwanjani baada ya kusumbuliwa na majeraha yaliyomuweka nje ya uwanja kwa kipindi fulani.

Nyota huyo anaamini bado ana mengi ya kuonyesha akiwa ndani ya kikosi cha Wekundu wa Msimbazi.

Bajaber alisema majeraha hayo yalikatisha kasi ya maendeleo yake kwa muda, lakini hakuwahi kupoteza matumaini ya kurejea katika kiwango kilichomfanya aangaziwe kabla ya kupata tatizo hilo.

Alieleza kuwa katika kipindi chote cha kuuguza majeraha amekuwa akifanya kazi kwa bidii na kujituma mazoezini ili kuhakikisha anarejea akiwa imara zaidi na tayari kulisaidia kikosi chake.

Mshambuliaji huyo amesema kiwango alichokionyesha akiwa na timu ya taifa ya Kenya ni ishara kuwa anaendelea kurejesha utimamu wake wa mwili pamoja na kujiamini, jambo ambalo linampa motisha ya kuendelea kupambana kwa ajili ya kupata nafasi Simba.

 

Akizungumzia mechi yake ya hivi karibuni akiwa na timu ya taifa, Bajaber alisema mafanikio ya kufunga mabao mawili na kutoa pasi moja ya bao ni uthibitisho kuwa juhudi zake zinaanza kuzaa matunda na kiwango chake kinaendelea kupanda siku hadi siku.

 

“Nilipitia kipindi kigumu kutokana na majeraha lakini sikuwahi kupoteza imani. Kufunga mabao mawili na kutoa asisti moja ni ishara kwamba ninaendelea kurejea kwenye kiwango changu,” alisema Bajaber.

 

Bajaber ameweka wazi kuwa lengo lake ni kufanya makubwa zaidi akiwa Simba na kuwathibitishia mashabiki uwezo wake halisi, ambao anaamini bado haujaonekana kikamilifu tangu ajiunge na klabu hiyo.

Kauli yake inakuja wakati Simba ikiendelea na maandalizi ya mechi zake muhimu za mwisho wa msimu, huku mashabiki wakitarajia kumuona akitoa mchango mkubwa katika harakati za timu hiyo kusaka mafanikio

JULIO ATAMBA ASEMA ANAIJUA YANGA KULIKO WENGI KOCHA WA MATAJI AFRIKA AINGIA KWENYE MPANGO MKAKATI WA YANGA