KIGOMA KUWAKA MOTO, YANGA SC WAJIPANGA KUVUNA POINTI 3 MBELE YA MASHUJAA
OFISA Habari wa Yanga SC, Ali Kamwe, amesema kikosi cha timu hiyo kimefika mjini Kigoma kikiwa katika hali nzuri na tayari kwa kazi, kuelekea mchezo wa raundi ya 26 wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Mashujaa FC.
Yanga SC inatarajiwa kushuka dimbani Juni 13, 2026 katika uwanja wa Lake Tanganyika Stadium, Kigoma, kusaka alama tatu muhimu zitakazowasaidia kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Kamwe amesema maandalizi yote muhimu yamekamilika kwa mafanikio, huku kikosi hicho kikiendelea na programu za mazoezi nyepesi ili kuhakikisha wachezaji wanakuwa tayari kikamilifu siku ya mchezo.
Amefafanua kuwa kufika mapema Kigoma kumewasaidia wachezaji wa Yanga SC kuzoea hali ya hewa na mazingira ya ugenini, jambo ambalo ni sehemu muhimu ya maandalizi ya mechi za ushindani mkubwa.
Kwa sasa, Yanga SC inaendelea kuongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara ikiwa na pointi 60, kila mchezo unaobaki unachukuliwa kama fainali katika mbio za kutetea ubingwa wao.
Aidha, Mashujaa FC wanatarajiwa kuingia kwenye mchezo huo wakiwa na faida ya uwanja wa nyumbani pamoja na hamasa ya mashabiki wao, jambo linaloifanya mechi hiyo kutajwa kuwa ngumu na ya ushindani mkubwa.
Kamwe amesema Yanga wanaiheshimu Mashujaa FC, lakini dhamira yao ni moja tukupata ushindi na kuondoka Kigoma wakiwa na pointi tatu muhimu.