JIMENEZ SHUJAA WA MEXICO ALIYENUSURIKA KIFO UWANJANI
Huenda Dunia isingemshuhudia mshambuliaji wa Mexico, Raul Jimenez akifunga bao la pili jana dhidi ya Afrika Kusini katika mechi ya ufunguzi wa Kombe la Dunia 2026 kutokana na changamoto aliyopata uwanjani miaka sita iliyopita.
Novemba 2020, mshambuliaji huyo hatari alipata jeraha baya lililohatarisha maisha yake wakati wa mechi ya Ligi Kuu England kati ya Wolverhampton na Arsenal.
Katika mchezo huo uliopigwa kwenye Uwanja wa Emirates, winga wa Arsenal, Willian alipiga kona kuelekea ndani ya eneo la hatari. Jiménez, alirudi nyuma kuongeza nguvu kwenye eneo la ulinzi ambapo alijikuta wakigombania mpira huo wa juu na beki wa Arsenal, David Luiz. Wachezaji hao wawili waligongana kwa nguvu vichwa kwa vichwa katika tukio lililowashtua wengi.
Kutokana na mashabiki kutoruhusiwa viwanjani wakati huo kwa sababu ya vizuizi vya ugonjwa wa Covid-19, sauti ya mgongano huo ilisikika wazi uwanjani. Wakati David Luiz akiinuka akiwa anatokwa damu, Jiménez alibaki amelala upande mmoja bila kuonyesha dalili zozote za kujitambua.
Kocha wa Wolves, Nuno Espírito Santo, pamoja na nahodha Conor Coady walitambua haraka uzito wa hali hiyo, huku madaktari wa timu wakikimbilia uwanjani na kutangaza hali ya dharura. Ilichukua zaidi ya dakika 10 kwa madaktari kumhudumia Jiménez, kumuongezea hewa ya oksijeni na kumuweka kwa uangalifu kwenye machela huku wakichukua tahadhari maalumu za kulinda uti wa mgongo kabla ya kukimbizwa hospitalini kwa matibabu zaidi.
Baada ya kukimbizwa hospitalini akiwa na mpasuko kwenye fuvu la kichwa pamoja na kutokwa damu nyingi ndani ya ubongo kufuatia mgongano huo mbaya, Jiménez alifanyiwa upasuaji wa dharura kuokoa maisha yake. Baadaye, madaktari walimweleza kuwa kuendelea kwake kuwa hai kulikuwa ni muujiza kutokana na uzito wa majeraha aliyoyapata.
Jiménez alieleza kuwa hakumbuki chochote kuhusu tukio hilo. Akiwa bado hospitalini, alitazama kwa mara ya kwanza video ya tukio lililomjeruhi kabla ya kuanza safari ndefu ya kupona.
Mshambuliaji huyo wa Mexico alitumia miezi tisa akipatiwa matibabu na kufanyiwa mazoezi maalumu ya kurejesha afya yake, katika mchakato uliokuwa na changamoto nyingi kabla ya kufanikiwa kurejea tena uwanjani.
Hata hivyo, madaktari walitoa tahadhari kwamba Jiménez asingeweza kucheza tena mpira kutokana na hatari kubwa ya kupata jeraha jingine kichwani ambalo lingeweza kusababisha madhara makubwa zaidi au hata kupoteza maisha.
Tahadhari hiyo ilitokana na ukubwa wa majeraha aliyokuwa ameyapata kwenye fuvu la kichwa na ubongo, hali iliyofanya kurejea kwake uwanjani kuonekana kuwa jambo lisilowezekana.
Baada ya miezi kadhaa ya matibabu na uchunguzi wa kina, madaktari walibaini kuwa mifupa ya fuvu lake ilikuwa imeungana kikamilifu, jambo lililopunguza kwa kiasi kikubwa hatari ya majeraha mengine.
Sambamba na hilo, matumizi ya vifaa maalumu vya kujikinga kichwani vilimsaidia kuongeza usalama wake, na hatimaye wataalamu wa afya wakampa ruhusa ya kurejea uwanjani.
Jiménez alirejea tena katika soka, Julai 17, 2021 alipoonekana hadharani kwa mara ya kwanza katika mchezo wa kirafiki wa maandalizi ya msimu dhidi ya Crewe Alexandra. Mshambuliaji huyo alianza mchezo huo na kucheza kwa dakika 34.
Mnamo Agosti 14, 2021 alianza kucheza rasmi akiwa na Wolverhampton akitumia dakika 90 katika mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu England msimu wa 2021/22 dhidi ya Leicester City.
Hatua nyingine muhimu katika safari yake ya kurejea ilifika Septemba 26, 2021, siku 336 tangu apate jeraha hilo baya, alipofunga bao lake la kwanza baada ya ajali hiyo.
Jiménez aliifungia Wolves bao pekee la ushindi dhidi ya Southampton, bao lililoashiria kurejea upya baada ya kipindi kigumu kilichotishia maisha yake ya soka.
Jiménez alikumbana na changamoto kubwa ya kurejesha kiwango chake cha zamani akiwa Wolves. Katika msimu wake wa mwisho wa Ligi Kuu England (2022/23), mshambuliaji huyo wa Mexico alishindwa kufunga bao lolote la ligi katika mechi 15 alizocheza.
Hali hiyo iliwafanya yeye pamoja na klabu kuamini kuwa kuondoka Molineux kungemsaidia kuondokana na presha kubwa aliyokuwa akiikabili na kumpa nafasi ya kuanza upya ili kurejesha kujiamini kwake.
Wakati huohuo, Wolves ilikuwa inakabiliwa na matatizo ya kifedha yaliyohusiana na kanuni za matumizi na mapato (FFP), jambo lililoilazimu klabu hiyo kuuza baadhi ya nyota wake wenye mishahara mikubwa akiwemo Jimenez ili kuepuka adhabu.
Jiménez aliondoka kwa kitita cha Pauni 5.5 milioni kwenda Fulham, huku majina mengine makubwa kama Rúben Neves, Conor Coady na Nathan Collins nayo yakiondoka. Kwa upande mwingine, Fulham ilikuwa katika harakati za kutafuta mshambuliaji mpya baada ya nyota wake Aleksandar Mitrović kufanya uhamisho wa kwenda Al-Hilal ya Saudi Arabia. Kocha Marco Silva alimwona Jiménez kuwa chaguo sahihi kutokana na uzoefu wake wa Ligi Kuu England na alikuwa tayari kumpa nafasi ya kucheza mara kwa mara, kitu ambacho Wolves haikuwa tena na uhakika wa kumpatia.
Hatua ya kujiunga na Fulham iligeuka kuwa mwanzo mpya wenye mafanikio makubwa kwa Jiménez. Baada ya kipindi kigumu, mshambuliaji huyo alifanikiwa kurejesha kiwango chake cha zamani akiwa chini ya kocha Marco Silva, akirejea kuwa mmoja wa washambuliaji tegemeo wa klabu hiyo ya London.
Katika msimu mmoja pekee akiwa Fulham, Jiménez alifunga mabao 14, rekodi iliyodhihirisha kurejea kwake kwa nguvu baada ya miaka ya maumivu na sintofahamu kuhusu mustakabali wake.
Mafanikio hayo yalimwezesha kuandika historia kwa kuwa mfungaji bora zaidi wa Mexico kuwahi kucheza Ligi Kuu England, akithibitisha kwamba alikuwa amefanikiwa kuushinda mtihani mkubwa zaidi katika maisha yake ya soka.
Baada ya kurejesha makali yake, aliwashawishi makocha wa Mexico kumrejesha katika mipango ya timu ya taifa kuelekea Kombe la Dunia la 2026, ambalo linaandaliwa kwa ushirikiano na Mexico.
Katika mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia dhidi ya Afrika Kusini kwenye Uwanja wa Azteca Juni 11, 2026, hadithi yake ya ukombozi ilikamilika. Dakika ya 66, Roberto Alvarado alipiga krosi nzuri ndani ya eneo la hatari na Jiménez, alifunga bao la kichwa lililoihakikishia Mexico ushindi wa mabao 2-0.
Baada ya kufunga, Jiménez alielekeza kidole chake angani kumuenzi baba yake, Raúl Jiménez Vega, aliyefariki dunia miezi mitatu iliyopita. Kufunga bao lake la kwanza kabisa katika historia ya Kombe la Dunia kwa mpira wa kichwa, mbele ya mashabiki wa nyumbani, baada ya kupona jeraha lililotishia maisha yake na kupitia majonzi ya kumpoteza baba yake, kulikamilisha safari ya miaka sita ya ukombozi kutoka kitanda cha hospitali hadi kuwa shujaa wa taifa la Mexico.