YANGA YATIKISA, BOKA AILETEA DOLLA 55,000
KLABU ya Yanga imeibuka mshindi katika shauri lililokuwa likiikabili klabu ya FC Lupopo ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), baada ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuiamuru FC Lupopo kuilipa Yanga jumla ya dola 55,000 za Marekani.
Sakata hilo linamhusu beki wa kimataifa wa DR Congo, Chadrack Boka, ambaye Yanga ilimsajili kutoka AS Real Kinshasa. Wakati wa usajili huo, AS Real Kinshasa ilieleza kuwa ilikuwa na umiliki kamili wa haki za mchezaji huyo, jambo lililoifanya Yanga kukamilisha mchakato wa usajili bila mashaka.
Hata hivyo, baadaye ilibainika kuwa FC Lupopo ilikuwa na madai ya umiliki wa haki za mchezaji huyo, hali iliyozua mgogoro kati ya pande hizo kuhusu malipo ya uhamisho wake.
Kutokana na hali hiyo, Yanga ililazimika kufanya malipo kwa AS Real Kinshasa ili kukamilisha usajili wa Boka, kabla ya kugundua kuwa kulikuwa na mgogoro wa umiliki wa mchezaji huyo.
Baada ya kupata taarifa hizo, klabu hiyo ya Jangwani ilifungua shauri FIFA ikiitaka FC Lupopo kurejesha fedha ilizopoteza kutokana na mkanganyiko huo.
Katika uamuzi wake, FIFA imekubaliana na hoja za Yanga na kuamuru FC Lupopo kulipa dola 50,000 ambazo Yanga ilidai pamoja na faini ya dola 5,000, na kufanya jumla ya dola 55,000.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, fedha hizo zinapaswa kulipwa ndani ya siku 45 tangu kutolewa kwa uamuzi huo, huku FIFA ikisisitiza utekelezaji wa maamuzi yake kwa wakati.
Uamuzi huo ni ushindi muhimu kwa Yanga, ambayo imeendelea kusimamia maslahi yake katika vyombo vya kimataifa, huku ikiongeza mafanikio nje ya uwanja baada ya kushinda kesi hiyo dhidi ya FC Lupopo.