Namungo FC

WATATU NAMUNGO WAITWA MEZANI

Vardo June 16, 2026 11:32 am

WAKATI Namungo ikibakiwa na mechi nne za kuhitimisha msimu wa 2025-2026 wa Ligi Kuu Bara, uongozi wa klabu hiyo umeanza mazungumzo na wachezaji wake watatu ili kuongeza mikataba baada ya hii ya sasa kukaribia kufikia ukomo.

Miongoni mwa wachezaji hao ni mkongwe, Jacob Masawe aliyeanza kucheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2010-2011 akiwa na Toto Africans ya jijini Mwanza na mkataba wake unamalizika mwisho wa msimu huu.

Masawe anayecheza nafasi mbalimbali ikiwemo beki wa kulia, kiungo mkabaji, kiungo mshambuliaji na mshambuliaji wa kati, ameonyesha kiwango kizuri tangu alipocheza pia Ndanda, African Lyon, Mwadui na Stand United.

Msimu huo wa 2010-2011, ulikuwa wa kihistoria kwa nyota huyo kwani licha ya kucheza Ligi Kuu kwa mara ya kwanza, pia alishinda tuzo ya mchezaji bora akiendeleza kiwango kizuri na hadi sasa ameifungia Namungo mabao mawili ya ligi.

Nyota mwingine aliyekuwa katika mazungumzo ya kuongezewa mkataba klabuni hapo ni mshambuliaji Mkongomani Heritier Makambo ambaye tangu ajiunge na Namungo Agosti 23, 2025 akitokea Tabora United kwa sasa TRA United, ameifungia bao moja tu.

Nyota huyo amewahi kutamba na Yanga, huku akiwa na uzoefu mkubwa baada ya kucheza DC Motema Pembe na St-Eloi Lupopo za kwao DR Congo, Horoya AC ya Guinea na Al-Murooj ya Libya.

Pia Hassan Kabunda aliyeifungia timu hiyo hadi sasa mabao mawili ya Ligi Kuu Bara, amewekewa mkataba mpya na kikosi hicho, baada ya huu wa sasa kuelekea mwishoni, huku akiwahi kuzichezea pia Ashanti United, Mwadui na KMC.

Akizungumza na Soka la Bongo, Mratibu wa Namungo, Ally Suleiman alisema; “Ni kweli mchakato huo umeanza lakini kama unavyojua hatupo sehemu salama sana na tunapigania kutoshuka daraja, suala hilo lipo ila mustakabali wa timu yetu wa kubakia Ligi Kuu ndio utakaotoa picha halisi ya wachezaji wote.”

YANGA YAITAKA AZAM FC ZANZIBAR KATIKA VITA YA UBINGWA MKENYA AWINDWA KAGERA SUGAR