MADAI YA KUBETI YAMPONZA ELYE WAHI KOMBE LA DUNIA
TORONTO, CANADA: MSHAMBULIAJI wa Ivory Coast, Elye Wahi mwenye umri wa miaka 23 amezuiwa kuingia Canada hivyo ataukosa mchezo wa Kombe la Dunia dhidi ya Ujerumani utakaochezwa Jumamosi ya Juni 20 jijini Toronto.
Wahi ambaye alianza katika kikosi cha ushindi wa Ivory Coast dhidi ya Ecuador mwishoni mwa wiki, anakabiliwa na tuhuma za kuhusika na upangaji wa matokeo ya mchezo kwa lengo la kunufaisha masoko ya ubashiri (spot-fixing) akiwa anaichezea Nice ya Ufaransa.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Marseille, mchezaji huyo alikamatwa mwezi uliopita katika uchunguzi unaohusu udanganyifu wa michezo, rushwa na utakatishaji fedha.
Inadaiwa Wahi alipata kadi ya njano kwa makusudi katika mechi ya Ligue 1 kati ya Nice na Metz mwezi Mei, tukio lililozua mashaka baada ya kuwepo kwa kiwango kikubwa cha dau zilizowekwa kuhusu tukio hilo.
Waandaaji wa Ligi Kuu ya Ufaransa (LFP) walithibitisha kuwa walipokea taarifa kuhusu idadi kubwa ya dau zilizowekwa zikihusisha kadi ya njano ya Wahi lakini hadi sasa hakuna hatua zozote za kinidhamu kutokana na uchunguzi unaoendelea.
Shirikisho la Soka la Ivory Coast (FIF) limesema halijapokea taarifa rasmi kuhusu mchakato wowote wa kisheria au kiutawala dhidi ya mchezaji huyo lakini limethibitisha kuwa hajapata vibali muhimu vya kuingia Canada.
Kutokana na hali hiyo, Wahi atabaki nchini Marekani akisubiri kurejea kwa kikosi hicho baada ya mchezo dhidi ya Ujerumani.
Baada ya kuivaa Ujerumani, Ivory Coast itacheza dhidi ya Curacao katika mchezo mwingine wa Kundi utakaofanyika Philadelphia wiki ijayo.
Uchunguzi dhidi ya Wahi unaendelea huku mamlaka za Ufaransa zikisema aliachiwa huru baada ya kuhojiwa lakini faili hilo bado halijafungwa.
Wahi anakuwa mchezaji wa pili katika Kombe la Dunia 2026 kuzuiwa kuingia Canada baada ya kiungo wa Ghana, Thomas Partey, kukataliwa visa kutokana na kesi za jinai zinazoendelea nchini Uingereza.