SIMBA YAPAMBANA HADI MWISHO, YALENGA KULA SAHANI MOJA NA YANGA
MENEJA wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema klabu hiyo bado ina imani kubwa ya kutimiza malengo yake makuu msimu huu kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Kombe la Shirikisho la CRDB.
Ahmed amesema licha ya Simba kuishia hatua ya nusu fainali mara tatu katika michuano mbalimbali iliyochezwa katika mikoa ya Mwanza, Mtwara na Manyara, bado wanaamini safari hii mambo yatakuwa tofauti kutokana na sapoti kubwa wanayotarajia kuipata kutoka kwa mashabiki wa Arusha.
Ameeleza kuwa Arusha imekuwa eneo lenye kumbukumbu nzuri kwa Simba katika nyakati muhimu, jambo linalowapa matumaini makubwa ya kufuzu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB. Kwa mujibu wake, ushirikiano na hamasa ya mashabiki itakuwa silaha muhimu katika kufanikisha lengo hilo.
“Simba inaendelea kupigania mataji mawili yaliyobaki msimu huu. Kama hatutafanikiwa kuchukua yote mawili, basi angalau moja lazima lirudi Msimbazi kutokana na ubora wa kikosi tulichonacho,” amesema Ahmed.
Ameongeza kuwa michuano ya Kombe la Shirikisho imefikia hatua muhimu, ikiwa imebakiwa na michezo miwili pekee kabla ya kumpata bingwa. Hivyo, wachezaji pamoja na benchi la ufundi wamejipanga kuhakikisha wanamaliza safari hiyo kwa mafanikio.
Akizungumzia mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Ahmed amesema Simba imekutana na changamoto mbalimbali katika msimu huu ambazo zimeathiri safari yao ya kuwania taji hilo, lakini bado hawajapoteza matumaini na wanaendelea kupambana hadi dakika ya mwisho.
Mbali na masuala ya uwanjani, Ahmed amewahamasisha Wanasimba wa Mererani kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuchukua kadi za uanachama,.
Amisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha klabu. Pia ameahidi kufuatilia kwa karibu zoezi hilo ili kuhakikisha kila Mwanasimba anapata nafasi ya kushiriki katika maendeleo ya timu yake.