Simba SC

SABABU YAFICHUKA MSIMU KUIKOSA SIMBA NUSU FAINALI

Vardo June 20, 2026 4:18 pm

KLABU ya Coastal Union imeweka wazi sababu za kutokuwepo kwa winga wake mahiri, Bakari Msimu, katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Simba SC utakaochezwa leo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Ufafanuzi huo umetolewa na Afisa Habari wa Coastal Union, Hussein Diego, kufuatia maswali na mijadala iliyozuka kuhusu kutokuwapo kwa baadhi ya nyota wa kikosi hicho kuelekea pambano hilo muhimu la kusaka tiketi ya fainali.

Kwa mujibu wa Diego, Msimu bado anasumbuliwa na jeraha la goti alilolipata akiwa kwenye majukumu ya timu ya taifa, hali iliyowalazimu viongozi na benchi la ufundi la Coastal Union kuchukua tahadhari kwa ajili ya kulinda afya na ustawi wa mchezaji huyo.

Amesema baada ya kurejea kutoka timu ya taifa, Msimu alifanyiwa vipimo na jopo la madaktari wa klabu, ambapo ilibainika kuwa hajafikia kiwango kinachomruhusu kucheza mechi za ushindani. Kutokana na hali hiyo, akaamuliwa kubaki Dar es Salaam akiendelea na matibabu badala ya kuambatana na kikosi kilichosafiri kwenda Arusha.

 

“Bakari Msimu kwenye mechi hii hatacheza kwa sababu alirejea kutoka timu ya taifa akiwa na majeraha ya goti. Kwa taratibu za timu na kwa ajili ya kumlinda mchezaji, tuliamua abaki Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu. Hatakuwepo kwenye mchezo dhidi ya Simba na pia dhidi ya TRA United,” amesema Diego.

Mbali na Msimu, Coastal Union pia itawakosa Christopher Oruchum na Meshack Mwamita, jambo linaloongeza changamoto kwa kikosi hicho kinachotarajia kuvaana na Simba SC katika mchezo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa. Mshindi wa pambano hilo atajihakikishia nafasi ya kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB.

SIMBA HAINA SABABU YA KUMWOGOPA MCHEZAJI YEYOTE, AHMED NEVES AINGIA KWENYE MOTO WA MASHABIKI WA RONALDO, APOTEZA WAFUASI MILIONI 2