Simba SC

SIMBA HAINA SABABU YA KUMWOGOPA MCHEZAJI YEYOTE, AHMED

Vardo June 20, 2026 4:13 pm

MENEJA wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema klabu hiyo haina sababu ya kuwaogopa wachezaji wa timu pinzani kutokana na ubora mkubwa wa kikosi ilichonacho kwa sasa.

Ahmed amesema kumekuwa na baadhi ya watu wanaojaribu kuichafua Simba kwa kuhusisha mafanikio yake na kutokuwepo kwa baadhi ya wachezaji wa timu wanazokutana nazo, klabu hiyo haihusiki kwa namna yoyote na maamuzi ya kiufundi yanayofanywa na wapinzani wake.

Amesema Simba imejijengea kikosi imara chenye uwezo wa kushindana katika kiwango cha juu, hivyo haina sababu ya kuhofu mchezaji yeyote.

“Kwa ubora tulionao Simba, tuwaogope Kelvin Nashon na Bakari Msimu? Wao wenyewe wanajua sababu za wachezaji wao kutocheza katika mechi husika. Sisi tuna timu bora sana na hatuhusiki na mambo hayo yanayoenezwa dhidi yetu,” amesema Ahmed.

Ameongeza kuwa nguvu na mafanikio ya Simba ndiyo yanayowafanya baadhi ya watu kuendelea kuizungumzia timu hiyo na kutafuta sababu mbalimbali za kupunguza thamani ya mafanikio inayoyapata uwanjani.

Ahmed ameitolea mfano mchezo dhidi ya Yanga uliochezwa Zanzibar, ambapo baadhi ya nyota hawakuwepo kikosini, akisema si sahihi kuhusisha kutokuwepo kwao na Simba. Amesisitiza kuwa kila timu ina mamlaka ya kufanya maamuzi yake ya ndani kuhusu uteuzi wa wachezaji na mipango ya mechi.

Kwa mujibu wa Ahmed, Simba kwa sasa imeelekeza nguvu zake katika kusaka matokeo chanya na kutimiza malengo yake makubwa ya msimu. Amesema kikosi hicho kimejengwa kwa kiwango cha kushindana katika michuano mikubwa ya kimataifa na kuwataka wanaokibeza kuacha kuipaka matope timu hiyo.

“Simba ina mipango yake ya kusaka matokeo na tuna timu yenye uwezo wa kushindana katika michuano mikubwa. Watesi wetu waache kutupaka matope na badala yake waangalie maendeleo ya timu zao,” amesema Ahmed.

SEKUNDE YA 65 YAIFUNGISHA VIRAGO UTURUKI SABABU YAFICHUKA MSIMU KUIKOSA SIMBA NUSU FAINALI