SEKUNDE YA 65 YAIFUNGISHA VIRAGO UTURUKI
CALIFORNIA, MAREKANI: PARAGUAY imefufua matumaini ya kutinga hatua ya 32 bora ya Kombe la Dunia 2026 baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Uturuki katika mchezo wa Kundi D uliochezwa asubuhi ya leo, Jumamosi, huko San Francisco Bay, California, Marekani.
Kilichoiumiza zaidi Uturuki siyo tu kupoteza mchezo huo, bali namna ilivyoshindwa kutumia nafasi nyingi ilizozitengeneza hata baada ya kucheza kipindi cha pili ikiwa na faida ya mchezaji mmoja kufuatia nyota wa Paraguay, Miguel Almirón, kutolewa kwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha kwanza.
Mchezo huo ulianza vibaya kwa Waturuki baada ya makosa ya pasi yaliyoigharimu timu hiyo ndani ya sekunde 65.
Galarza alitumia mwanya huo kuachia shuti lililomshinda kipa Ugurcan Cakır na kuandika bao ambalo baadaye liligeuka kuwa la ushindi.
Baada ya bao hilo, Uturuki ilitawala sehemu kubwa ya mchezo. Nyota wao, Arda Güler, alipata nafasi ya kwanza dakika ya 14 lakini akapiga juu ya lango.
Dakika zilivyozidi kwenda mashambulizi yaliongezeka huku Kenan Yıldız akijaribu kufunga kwa kisigino, lakini kipa Orlando Gill akaokoa kirahisi.
Nafasi bora zaidi ya kipindi cha kwanza ilikuwa dakika ya 31 wakati kichwa cha Mert Muldur kilipogonga mwamba na baadaye kutoka nje, tukio lililoonyesha jinsi bahati ilivyokuwa upande wa Paraguay.
Mambo yalibadilika zaidi dakika chache kabla ya mapumziko baada ya Almirón kupewa kadi nyekundu baada ya kuziba mdomo wake alipokuwa akizungumza na mpinzani. Uamuzi huo uliiacha Paraguay na wachezaji 10 kwa zaidi ya dakika 45 zilizobaki.
Wengi walitarajia Uturuki kurejea kwa nguvu kipindi cha pili, lakini licha ya kutawala mpira na kutengeneza nafasi kadhaa, walishindwa kabisa kuvunja ukuta wa Paraguay.
Matokeo hayo yanaifanya Uturuki kupoteza mechi ya pili mfululizo na rasmi kuaga mashindano hayo licha ya kurejea Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza baada ya miaka 24. Mchezo wao wa mwisho dhidi ya Marekani sasa utakuwa wa kutimiza ratiba.
Kwa upande wa Paraguay, ushindi huo umewafanya kuwa na matumani ya kwenda hatua ya mtoano kama wataibuka na ushindi katika mchezo wao wa mwisho dhidi ya Australia ambao nao wanapointi tatu.