MAGORI AFUNGUKA MPANGO WA SIMBA, RIPOTI YA BARKER YAINGIA KAZINI
MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba SC, Crescetius Magori, amesema klabu hiyo tayari imeanza maandalizi ya kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu ujao baada ya kupokea ripoti kutoka kwa Kocha Mkuu, Steve Barker, iliyobainisha maeneo yanayohitaji maboresho katika dirisha kubwa la usajili.
Magori amesema bodi imeanza kufanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa na kocha huyo kwa kufuatilia wachezaji waliopendekezwa pamoja na nafasi zinazohitaji kuongezewa nguvu ili kuongeza ushindani ndani ya kikosi.
Ameeleza kuwa hatua ya Simba kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB kwa mara ya kwanza baada ya miaka mitatu ya kuishia robo fainali ni ishara kuwa mabadiliko yaliyofanywa ndani ya timu yameanza kuonyesha matokeo chanya.
“Tunashukuru tumefanikiwa kuingia fainali baada ya miaka mitatu kuishia katika hatua ya robo fainali. Hii inaonyesha kuwa timu mpya tuliyoijenga imeweza kutufikisha hapa tulipo,” amesema Magori.
Kwa mujibu wa Magori, bodi imefanya tathmini ya kina ya kikosi cha sasa na imejipanga kufanya maboresho zaidi ili kuhakikisha Simba inakuwa na kikosi imara zaidi kitakachoweza kushindana kwa mafanikio katika mashindano ya ndani na ya kimataifa.
“Bodi tumekaa na kuangalia kwa kina mahitaji ya timu. Tunatarajia kufanya maboresho zaidi ili Simba iwe bora zaidi kuliko ilivyo sasa,” amesema.
Amesisitiza kuwa utekelezaji wa ripoti ya Barker tayari umeanza, huku lengo kuu likiwa ni kusajili wachezaji wenye ubora na uwezo wa kuongeza nguvu katika maeneo yaliyoonekana kuhitaji maboresho.
Magori pia amepongeza usajili uliofanywa katika dirisha dogo la usajili, akibainisha kuwa baadhi ya nyota waliosajiliwa wameonyesha kiwango kizuri na kutoa mchango mkubwa ndani ya timu. Miongoni mwao ni Anicet Oura, Libasse Gueye na Inno Loemba ambao wamekuwa sehemu muhimu ya mafanikio ya Simba katika kipindi cha hivi karibuni.