Yanga SC

UBINGWA WA TANO MFULULIZO WAWAVUTA YANGA KIRUMBA

Vardo June 21, 2026 10:02 am

UONGOZI wa Yanga SC umeweka wazi kuwa lengo lao kuu kwa sasa ni kuhakikisha wanalitetea kwa mafanikio taji la Kombe la Shirikisho la CRDB, huku wakijiandaa kwa mchezo muhimu wa nusu fainali dhidi ya Azam FC.

Yanga itashuka dimbani leo Jumapili, Juni 21, 2026 katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kusaka tiketi ya kutinga fainali ya michuano hiyo.

Mshindi wa pambano hilo atakutana na Simba SC katika mchezo wa fainali unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Akizungumza kuelekea mchezo huo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ali Kamwe, amesema klabu hiyo imejipanga kikamilifu kuhakikisha inalinda heshima ya ubingwa iliyonayo kwa sasa.

Kamwe amesema Kombe la Shirikisho la CRDB bado lipo mikononi mwa Yanga kama mabingwa watetezi, hivyo dhamira ya kila mmoja ndani ya klabu ni kuona timu hiyo inalitetea na kutwaa ubingwa kwa mara ya tano mfululizo.

Amesisitiza kuwa mafanikio hayo hayawezi kupatikana bila mchango mkubwa wa mashabiki, akiwataka Wananchi kujitokeza kwa wingi katika Uwanja wa CCM Kirumba ili kuwapa hamasa na nguvu wachezaji wao wakati wa pambano hilo muhimu.

“Kombe la Shirikisho la CRDB kwa sasa lipo mikononi mwetu kama mabingwa watetezi. Dhamira yetu sote ni kuona Yanga inalitetea taji hili na kutwaa ubingwa kwa mara ya tano mfululizo. Hata hivyo, azma hiyo haitafikiwa kwa urahisi bila sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wetu,” amesema Kamwe.

Amesema ratiba ya mashindano imekuwa ngumu na yenye msongamano mkubwa, jambo linalofanya kila mchezo uliobaki kuwa wa muhimu sana.

Kutokana na hali hiyo, amewataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi na kuendelea kuwa bega kwa bega na timu yao katika safari ya kutetea ubingwa huo.

“Kwa pamoja, tuonyeshe nguvu ya Wananchi na tuwe sehemu ya safari ya kuelekea kutetea ubingwa wetu,” ameongeza.

SIMBA WAPELEKA UJUMBE MZITO YANGA NA AZAM KABLA YA FAINALI MAGORI AFUNGUKA MPANGO WA SIMBA, RIPOTI YA BARKER YAINGIA KAZINI