HUU SI WAKATI WA KUKATA TAMAA, HUU NI WAKATI WA KUPAMBANA, KAMWE
BAADA ya kuondolewa katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, amewataka mashabiki wa klabu hiyo kuendelea kuiamini timu na kubaki wamoja katika harakati za kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga ilimaliza safari yake kwenye michuano hiyo baada ya kufungwa mabao 3-2 na Azam FC katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, matokeo yaliyowavunja moyo wengi wa mashabiki wa timu hiyo.
Akizungumza baada ya mchezo huo, Kamwe alisema licha ya maumivu ya kuondolewa kwenye mashindano hayo, bado Yanga ina nafasi kubwa ya kutimiza moja ya malengo yake makuu msimu huu kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Alieleza kuwa timu hiyo imebakiza mechi tatu muhimu ambazo zitakuwa na mchango mkubwa katika kuamua hatima ya mbio za ubingwa, hivyo ni muhimu kwa kila Mwanayanga kuendelea kutoa sapoti kwa kikosi hicho.
“Matokeo ya mchezo wa Kombe la Shirikisho yametuumiza wadau wengi wa Yanga, lakini huu si wakati wa kukata tamaa. Huu ni wakati wa kuonyesha mshikamano na kuipa timu nguvu ya kupambana hadi mwisho wa msimu,” alisema Kamwe.
Amesema maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC tayari yameanza, huku akisisitiza kuwa kikosi hicho kina nafasi nyingine ya kuonyesha uwezo wake katika dakika 90 zitakazochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Kamwe pia aliwataka mashabiki wa Yanga waliopo Zanzibar, Unguja na Pemba kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu siku ya Jumatano, akieleza kuwa uwepo wao uwanjani unaweza kuwa chachu muhimu katika safari ya kutetea ubingwa.
“Mashabiki wetu wanahitajika zaidi katika kipindi hiki. Tunahitaji kuwa kitu kimoja, kuwa na morali moja na kupambana pamoja hadi mwisho,” amesisitiza.
Yanga itaingia katika mchezo huo ikiwa na lengo la kurejea kwenye njia ya ushindi na kuendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu mwingine mfululizo.