ISMAIL TOURE NI MTU KAZI HASA
YULE beki wa kati wa Simba, Ismail Toure ni kitasa sana na kijiwe kinakoshwa sana uchezaji wake.
Anakaba vizuri bila kucheza rafu, anaweza kuichezesha timu kuanzia nyuma, pia ana kasi, nguvu na hesabu nzuri pindi timu inaposhambuliwa.
Ni ingizo la Simba dirisha dogo la usajili akiwa pendekezo la Kocha Mkuu wa timu hiyo, Steve Barker.
Simba kwa sasa ametengeneza pacha nzuri sana na nahodha msaidizi wa timu hiyo, Rushine De Reuck na kwa hakika wamesaidia kuiongezea uimara mkubwa timu hiyo ktika safu ya ulinzi.
Kwa dalili zilivyo, kuna uwezekano mkubwa Simba ikaendelea kubaki naye kwa muda mrefu zaidi kwani ndani ya miezi mitano ambayo ameichezea, tayari ameshaonesha kitu na amekuwa na msaada mkubwa kwao.
Hakuna sababu ya msingi kwa Simba kuanza kutafuta beki mpya wa kati na kuachana na Toure wakati tayari ameshazoea mazingira ya Tanzania na anafanya vizuri ndani ya uwanja.
Toure ni mfano halisi wa namna mchezaji anayesajiliwa katika dirisha dogo la usajili anatakiwa awe, kutokana na mahitaji halisi ya muda huo kulinganisha na ule wa dirisha kubwa.
Mchezaji anayesajiliwa katika dirisha dogo la usajili anapaswa kuingia moja kwa moja katika timu na kuleta matokeo chanya badala ya kuhitaji tena muda wa kumudu mazingira na ushindani wa ndani ya timu.
Anayesajiliwa dirisha kubwa anaweza kidogo kuhitaji muda kwa vile atapata fursa ya kuwa pamoja na timu katika maandalizi ya msimu mpya.