Simba SC

MO DEWJI NA BARKER WAKETI MEZANI, USAJILI WAPEWA KIPAUMBELE

Vardo June 26, 2026 10:22 am

KATIKA kuhakikisha Simba inakuwa na kikosi imara zaidi msimu wa 2026/27, Bilionea na Mfadhili wa klabu hiyo, Mohamed Dewji (Mo), anatarajiwa kufanya kikao muhimu na benchi la ufundi linaloongozwa na kocha Steve Barker pamoja na Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo kujadili mipango ya kuijenga timu.

Taarifa zinaeleza kuwa Mo tayari yupo nchini na katika siku chache zijazo ataanza vikao vya ndani vitakavyolenga kupanga mkakati wa usajili wa wachezaji wapya pamoja na maboresho mengine yatakayokiwezesha kikosi hicho kuwa na ushindani mkubwa ndani na nje ya Tanzania.

Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika, ajenda kubwa ya kikao hicho itakuwa ni kujadili maeneo yanayohitaji kuimarishwa, aina ya wachezaji wanaotakiwa kusajiliwa na namna ya kukiandaa kikosi kwa ajili ya mashindano ya msimu ujao.

“Uongozi wa Simba umejipanga kufanya maboresho makubwa katika maeneo yenye uhitaji ili kuhakikisha timu inakuwa na ushindani mkubwa zaidi katika Ligi Kuu Tanzania Bara na michuano ya kimataifa,” kilisema chanzo hicho.

Mbali na usajili wa wachezaji wapya, taarifa hizo zinaeleza kuwa Mo pia atazungumza na kocha Steve Barker kuhusu mustakabali wake ndani ya klabu, huku uongozi ukionesha nia ya kuendelea naye msimu ujao ili kutekeleza malengo waliyojiwekea.

Hatua ya Mo kushiriki moja kwa moja katika maandalizi ya msimu mpya imeongeza matumaini kwa mashabiki wa Simba, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakisubiri kuona timu yao ikifanya usajili wa nyota wenye uwezo wa kuirejesha kwenye mafanikio makubwa.

Iwapo mipango hiyo itatekelezwa kama ilivyopangwa, dirisha hili la usajili linatarajiwa kuwa miongoni mwa yenye ushindani mkubwa, huku Simba ikionyesha dhamira ya kujenga kikosi chenye uwezo wa kupambana kwa mataji yote itakayoshiriki msimu wa 2026/27

YANGA YAKATAA KUSHINDWA, YAITANGAZIA PRESHA SIMBA FAINALI YA SHIRIKISHO ISMAIL TOURE NI MTU KAZI HASA