Yanga SC

YANGA YAKATAA KUSHINDWA, YAITANGAZIA PRESHA SIMBA FAINALI YA SHIRIKISHO

Vardo June 26, 2026 9:58 am

BAADA ya kukamilisha kampeni yake ya Ligi Kuu Tanzania Bara, uongozi wa Yanga umesema utaelekeza nguvu zake zote kuisapoti Azam FC katika fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Simba, huku ukisisitiza kuwa hautaiacha timu hiyo ipambane peke yake.

Msemaji wa Yanga, Ali Kamwe, amesema mpango huo utaanza mara baada ya timu hiyo kumaliza rasmi majukumu yake ya ligi ifikapo Juni 30, 2026, ikiwa tayari imekamilisha lengo lake la kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kamwe amesema Yanga inaamini kuwa baada ya kutimiza malengo yake ya msimu, ni wakati wa kuielekezea nguvu Azam FC ili iweze kutoa upinzani mkali dhidi ya Simba katika pambano la kusaka taji la Kombe la Shirikisho la CRDB.

Amesisitiza kuwa sapoti hiyo haitakuwa ya mashabiki pekee, bali ni msimamo wa klabu nzima, ambapo viongozi, wanachama na wapenzi wa Yanga watashiriki kwa namna mbalimbali kuhakikisha Azam FC inapata morali ya kupambana.

“Tukimaliza Ligi Kuu Tanzania Bara Juni 30, 2026 na tumeshakuwa mabingwa, baada ya hapo tutaelekeza nguvu zetu kuwasapoti Azam FC katika mchezo wao wa fainali dhidi ya Simba.

 

Tutajitoa kwa kila hali, si kwa mashabiki pekee, bali tutaweka nguvu yetu kubwa katika fainali hiyo ya Kombe la Shirikisho la CRDB kumsaidia Azam FC kutwaa kombe hilo dhidi ya Simba,” amesema Kamwe.

Kauli hiyo imeibua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau wa soka nchini, huku baadhi wakiitafsiri kama sehemu ya mwendelezo wa ushindani wa jadi kati ya Yanga na Simba, na wengine wakisubiri kuona namna ambavyo sapoti hiyo itajidhihirisha siku ya mchezo.

Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB inatarajiwa kuchezwa Julai 4, 2026, kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba, ambapo Azam FC na Simba zitakutana katika pambano la kuwania taji, mchezo unaotarajiwa kuvuta hisia kubwa kutoka kwa mashabiki wa soka nchini

NI AZIZ KI AU MASHINE HII YA KAZI KUTOKA UGANDA…MMOJA LAZIMA ATUE JANGWANI…. MO DEWJI NA BARKER WAKETI MEZANI, USAJILI WAPEWA KIPAUMBELE