KWENYE RADA ZA SIMBA KIHIMBWA AHUSISHWA……….
KIUNGO mshambuliaji wa Mashujaa, Salum Kihimbwa ni kati ya wachezaji wanaotajwa kufanya mazungumzo na viongozi wa Simba kwa ajili ya kuongezwa katika kikosi hicho msimu ujao wa 2026/27.
Ingawa msimu huu alisumbuliwa na majeraha ya hapa na pale, tofauti na msimu uliopita wa 2024/25 aliomaliza akiwa na mabao manne na asisti tano akiwa na Fountain Gate, hali hiyo haijawazuia viongozi wa Simba kuona ni miongoni mwa wazawa wenye viwango vizuri.
Mwanaspoti lilipata taarifa za ndani kutoka Simba zilizosema yamefanyika mazungumzo ya awali ambayo kwa asilimia kubwa hayana pingamizi kwa upande wa mchezaji, na sasa ni juu ya uongozi kukamilisha mchakato huo.
Endapo dili hilo litakamilika, Kihimbwa anayeweza kucheza kama winga wa kulia, kushoto na pia namba 10 atakwenda kukutana na ushindani mkali wa mastaa wa kigeni kama Clatous Chama aliye na mabao manane na asisti saba, Libasse Gueye mwenye mabao saba na Anicet Oura mwenye mabao matano na asisti tatu.
Chanzo hicho kilisema: “Simba tunasajili kikosi cha mchanganyiko cha vijana na wachezaji wenye uzoefu. Ingawa Kihimbwa bado hajasaini, mazungumzo yamefanyika na yalifika pazuri.”
Ameongeza: “Siyo Kihimbwa pekee, kuna wachezaji wengi ambao viongozi wanazungumza nao. Ukimya uliokuwepo ni kutokana na majukumu ya mechi za mwishoni ambazo zimebeba malengo makubwa ya klabu.”
Alipotafutwa Kihimbwa, ambaye mtandao wa Transfermarkt unamuonyesha alizaliwa Desemba 12, 1997, ili kuthibitisha taarifa hizo amesema:
“Akili yangu kwa sasa ni kumaliza msimu kwa kuona timu ninayoichezea inapata matokeo mazuri. Mambo mengine siyo wakati wake na siwezi kuzungumzia chochote.”
Wachezaji wazawa wanaotajwa pia kuhusishwa na mipango ya Simba ni Kelvin Nashon wa Pamba Jiji aliye kwa mkopo kutoka Singida Black Stars, huku mkataba wake ukitarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu, pamoja na Bakari Msimu kutoka Coastal Union ya Tanga.